……….
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdullah amesema Serikali inaendelea kuunga mkono miradi ya maendeleo inayoanzishwa na Taasisi mbalimbali ili kuboresha huduma kwa Wananchi.
Ameyasema hayo wakati alipokuwa akifunguwa Bonaza la Afya, lililoandaliwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita na kujumuisha matembezi kutoka Kiembesamaki hadi Kiwanja cha Kizingo Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi anahimiza ubunifu katika Taasisi hivyo amempongeza Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita kwa kuanzisha Tamasha hilo muhimu.
Aidha ameahidi kuunga mkono miradi yote ya maendeleo inayoanzishwa kwa ajili ya kuwaondoshea changamoto wanajamii ikiwemo matatizo ya Afya.
Kwa uapande wake Muandaaji wa Bonaza hilo ambae pia ni Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita amesema lengo la kuanzisha Bonaza hilo ni kuunga Mkono juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika kuwapatia Wananchi huduma bora za Afya.
Amesema wameanzisha Bonaza hilo kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wanaosumbuliwa na matatizo mbalilmbali ikiwemo ya Ngozi, Macho, Meno na Maradhi yasioambukiza kama vile Kisukari na Sindikizo la Damu.
Hata hivyo Mhe. Tabia amesema wanatagemea kuanzisha Matamasha mbalimbali ikiwemo ya Michezo na kuwashirikisha Wasanii wa Zanzibar ili waweze kuhamasisha jamii na kupata Ajira.
Mwakilishi wa Viti Maalum Mkoa wa Magharibi kichama Mhe. Fatma Ramadhan Mandoba na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Mkoa wa Mjini Kichama Fransisca …wamesema Afya ni Msingi wa Maisha na bila ya Afya hakuna maisha hivyo wametoa wito kwa Wananchi kulipokea Bonaza hilo sambamba na kuwashauri Wadau wengine wa Afya kuiga mfano wa Mhe. Tabia.
Kwa upande wake Asyah Ramadhan Khamis Mwenyekiti wa Chama Cha Wanafunzi Madaktari kutoka Chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar (TAMSA SUZA) amesema wameamua kufikisha huduma hizo kwa jamii ili ziweze kuwasaidia.
Pamoja na hilo amesema Bonaza hilo, litasaidia Wananchi kujuwa Afya zao ili waweze kujikinga na kupata matibabu endapo watabainika kuwa na matatizo ya kiafya.
Uzinduzi wa Bonaza la Afya, limeandaliwa na Wizari wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kushirikiana na Chama cha Wanafunzi wa Madaktari TAMSA SUZA na Wizara ya Afya Zanzibar na kujumuisha matembezi kutoaka Kiembe Samaki hadi Kiwanja cha Kizingo, Upimaji wa Afya na Uchangiaji wa Damu.