….,………….
Na Sixmund Begashe
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema ujio wa Watafiti wa Mimea Vamizi kutoka nchini Cuba waliokuja nchini watasaidia katika kukabili Mimea Vamizi katika Hifadhi ya Taifa Saanane pamoja na Ziwa Viktoria ambayo yamekuwa changamoto katika Shughuli za usafirishaji, Uvuvi na Utalii.
Mhe. Mtanda amebainisha hayo Februari 24, 2025 mara baada ya kuipokea timu ya Watafiti wa Mimea vamizi kutoka Jamhuri ya Cuba walioungana na Wataalamu wa Ikolojia kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii ambao wametembelea mwambao wa Ziwa Viktoria eneo la Kigongo Busisi pamoja na Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saa Nane ambapo amesema ujio wa wao utaleta suluhu ya tatizo la Magugu ya maji katika Ziwa hilo kubwa na katika Hifadhi hiyo ya kipekee Duniania.
“Tumefurahi kupata huu ugeni wa Watafiti wa Mimea Vamizi kutoka Cuba, ambao wameandaliwa kuja na Wizara ya Mambo ya Nje kupitia Balozi wetu wa Tanzania Mhe. Balozi. Humphrey Polepole na Wizara ya Maliasili na Utalii kwani wamekuja wakati muafaka kwakuwa hivi karibuni kuna gugu vamizi linazaa mara kwa mara na kwa muda mfupi ziwa limekuwa linafunikwa kwahiyo huathiri miundombinu ya usafirishaji na samaki wa Vizimba”- Alieleza Mkuu wa Mkoa Mtanda
Aidha ameeleza kuwa Magugu vamizi yanaweza kuleta athari kwa wafugaji wa Samaki kwa njia ya vizimba hivyo serikali imeleta wataalamu hao katika muda muafaka.
“Sasa hivi Ziwa Viktoria tunafuga samaki kwa vizimba na kuna vizimba takribani 1047, kwahiyo endapo gugu vamizi litaendelea kusambaa katika maeneo mengine litaleta athari kiuchumi, kwa vijana wafugaji ndio maana tunaishukuru serikali kwa kuwaleta Wataalamu haraka kabla hawajaathirika”-aliongeza Mhe. Mtanda.
Afisa Mistu Mkuu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mwenyekiti ziara ya timu ya watafiti mimea vamizi kutoka Jamhuri ya Cuba na Tanzania Bw. Emmanuel Msofe amasema sekta mbalimbali zimeathiriwa na Mimea Vamizi hususani katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria hivyo ziara ya Watafiti hao inatarajiwa kuleta neema katika Mkoa wa Mwanza na Tanzania kwa ujumla.
Naye Kaimu Mkuu Hifadhi ya Kisiwa cha Saa Nane Afisa Mhifadhi Mkuu Pellagy Marandu ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kukuza sekta ya utalii ikiwemo kuleta Watafiti hao ambao watakuwa msaada mkubwa katika kutatua tatizo hilo ambalo limekuwa kero ya mara kwa mara katika mageti ya kuingilia Hifadhini na kutoka.
Timu ya Watafiti wa Mimea vamizi kutoka Jamhuri ya Cuba walioungana na Wataalamu wa Ikolojia kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii inatarajiwa kuleta suluhu ya tatizo la mimea vamizi katika maeneo yaliyohifadhiwa pamoja vyanzo vya maji kwa lengo la kuleta ustawi wa sekta mbalimbali zinazoathiriwa nachangamoto hiyo.