Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed (wapili kutoka kushoto) akimkabidhi Kaimu Meneja Mkuu Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme nchini (ETDCO) CPA. Sadock Mugendi (watatu kutoka kushoto) Tuzo ya Mshindi wa kipengele cha Mkandarasi Bora wa Ujenzi wa Miundombinu ya Umeme kutoka Zanzibar International Construction Awards (ZICA) , Afisa Uhusiano ETDCO Bi. Samia Chande (wakwanza kushoto) katika hafla ya ugawaji tuzo zilizofanyika Februari 22, 2025, Zanzibar.
Wafanyakazi wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme nchini (ETDCO) wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukabidhiwa tuzo ya mshindi wa kipengele cha Mkandarasi Bora wa Ujenzi wa Miundombinu ya Umeme kutoka Zanzibar International Construction Awards (ZICA).
………..
Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme nchini (ETDCO) imebuka mshindi katika kipengele cha Mkandarasi Bora wa Ujenzi wa Miundombinu ya Umeme, katika Tuzo za Zanzibar International Construction Awards (ZICA) zilizofanyika Februari 22, 2025, Zanzibar.
Akizungumza wakati akikabidhi Tuzo kwa Washindi, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed, amesema kuwa sekta ya ujenzi ni msingi mkuu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, huku akiwataka washiriki wote kutumia tuzo hizo kama chachu ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kufikia viwango vinavyohitajika na kuleta tija kwa Taifa.
Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO CPA. Sadock Mugendi, ameishukuru ZICA kwa kutambua mchango wao katika sekta ya ujenzi wa miundombinu ya umeme nchini, na kuahidi kuendelea kutoa huduma zenye viwango ili kukuza uchumi wa nchi.
“ETDCO tumejipanga kuhakiksha tunaboresha matumizi ya teknolojia kwa kununua mashine za kisasa pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu ili kufikia viwango vinavyohitajika kimataifa” amesema CPA. Mugendi
CPA. Mugendi ameeleza kuwa ETDCO ni kampuni iliyopewa jukumu la kutekeleza miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umeme kupitia wadau mbalimbali ikiwemo TANESCO, REA pamoja na makampuni binafsi.
Katika Tuzo za ZICA kilikuwa na washiriki 150 na ETDCO miongoni mwa washindi 30 waliotunukiwa tuzo hizo kutokana na ufanisi wa kazi pamoja na juhudi katika kuhakikisha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme inakuwa bora na salama ili watanzania waweze kupata umeme wa uhakika wakati wote na kupelekea kuchochea maendeleo ya uchumi kwa wananchi.