Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Brazil zimeelezea dhamira ya kuendelea kukuza ushirikiano katika sekta ya ulinzi kwa lengo la kujenga uzoefu, ujuzi, umahiri na usalama kati ya mataifa hayo na kuleta ufanisi katika uenyeji wa matukio makubwa sambamba na usimamizi wa majanga.
Msisitizo huo umetolewa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda alipofunga mafunzo ya masuala ya ulinzi, michezo, utalii na matukio makubwa yaliyoendeshwa na Jeshi la Zimamoto la Serikali ya Brazil kwa askari wa Tanzania.
Balozi Kaganda alisema dunia ya sasa imejaa matukio yanayohitaji ufanisi katika kuyatatua hivyo ni wakati sahihi wa kujenga uwezo na kubadilishana uzoefu kwa vyombo vya ulinzi ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika usimamizi wa maeneo ya mikusanyiko mikubwa.
‘’Ukitembea duniani watu wamekuwa wakishuhudia umahiri wetu katika kusimamia uenyeji wa matukio mbalimbali ambapo,sifa hizi zinatokana na Diplomasia imara inayoongozwa na Mwanadiplomasia namba moja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tunamshukuru kwa kuifanya nchi yetu kuwa kituo cha mikutano ya kimataifa na mashindano makubwa ya michezo’’, alisisitiza Balozi Kaganda.
Kufuatia umahiri huo Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza logo za ndani- CHAN itakayofanyika baadaye mwaka huu 2025, michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika- AFCON itakayofanyika mwaka 2027 na Mkutano wa Kimataifa wa Nyuki 2027.
Amesema mafunzo hayo ni fursa muhimu kwakuwa Brazil imeshakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Nchi 20 tajiri duniani (G20)- 2024, michuano ya kombe la Dunia (FIFA World Cup-2014) na mashindano ya Olympic duniani – 2016.
Naye, Mratibu wa mafunzo hayo ya kijeshi wa Serikali ya Brazil, Douglas Julio amewashukuru askari wa Jeshi la Zimamoto la Brazil kwa kuja Tanzania na kufanikisha kujenga ujuzi wa masuala ya ulinzi katika mikusanyiko mikubwa ya watalii, mawasiliano ya kimkakati wakati wa hali ya dharura, ubunifu na matumizi ya teknolojia ya kisasa. Ameongeza kuwa hayo yote yataiweka nchi katika hali ya usalama na kuvutia uwekezaji na biashara za kimataifa.
Wakati huo huo, Mratibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi nchini, Apolnary Mwakagamba ambaye alishiriki mafunzo hayo ameeleza kuwa washiriki wamejifunza namna Brazil ilivyowekeza katika kukabiliana na majanga na usimamizi wa matukio makubwa kwa mafanikio licha ya ukubwa wa miji yake na uwingi wa watu katika maeneo ya fukwe, viwanja vikubwa vya michezo na majengo yanayotumika kwa shughuli za kimataifa.
Askari 173 kutoka Jeshi la Zimamoto, Jeshi la Polisi na Jeshi la Uhamiaji ambapo wamejengewa uelewa na uzoefu katika mada za usimamizi wa majanga, ukoaji wa maisha, kuisaidia Serikali katika nyakati za dharura mfano, ajali za umeme, maporomoko ya ardhi na ajali za kuanguka kwa majengo na kuwekewa mpango maalum wa kukabiliana na dharura.
Tanzania na Brazil zinashirikiana katika sekta za kilimo, afya, biashara, uwekezaji, utalii, elimu na usalama ambayo ni miongoni mwa sekta mpya za ushirikiano zinazoendelea kukua katika ushirikiano huo.