Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, akihutubia wakati wa uzinduzi wa mfumo jumuishi wa viwango (IQMST).
Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, akimkabidhi cheti cha shukrani, muanzilishi na msimamizi wa mfumo wa jumuishi wa viwango (IQMST) ulioandaliwa na Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS).
MAKAMU wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, akisaini bango maalum alipowasili katika ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa ndege, Zanzibar kuzindua mfumo wa jumuishi wa viwango (IQMST) ulioandaliwa na Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS).
………………….
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema kuwa serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani na nje ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakidhi viwango vya kikanda na kimataifa.
Hemed alitoa kauli hiyo jana kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, wakati wa uzinduzi wa Mfumo Jumuishi wa Kielektroniki wa Viwango wa Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) katika hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege Zanzibar.
Akifafanua kuhusu mfumo huo, Hemed alisema kuwa Mfumo wa Viwango wa ISQMT utaimarisha usimamizi wa ubora wa bidhaa zinazozalishwa au kuingizwa nchini, kulinda afya na usalama wa wananchi, na kukuza ushindani wa bidhaa za Zanzibar katika masoko ya kikanda na kimataifa.
“Mfumo huu utaongeza ufanisi katika sekta ya viwanda na biashara, kuchochea maendeleo ya uchumi, na kuondoa changamoto zilizokuwepo awali, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma kwa uwazi na kwa ufanisi zaidi,” alisema.
Aidha, aliagiza taasisi za serikali kutekeleza agizo la kuanzisha mifumo ya kielektroniki ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi. Pia, aliwataka wafanyabiashara, wazalishaji, na wadau wa sekta ya viwango kutumia mfumo huo kikamilifu kwa lengo la kuboresha ubora wa bidhaa na kuhakikisha viwango vinadhibitiwa nchini.
Makamu wa Pili wa Rais pia aliwataka watendaji wa ZBS kuhakikisha kuwa Mfumo wa ISQMT unatumika ipasavyo na kuhamasisha taasisi nyingine kuiga mfano huo kwa maendeleo ya sekta ya viwango.
Aidha, aliipongeza Taasisi ya Kuendeleza Biashara Afrika (TradeMark Africa – TMA) Kanda ya Afrika Mashariki kwa kusaidia upatikanaji wa mfumo huo na kuiomba iendelee kusaidia taasisi nyingine za serikali katika kuanzisha mifumo ya kidijitali ili kuboresha utoaji wa huduma.
Kwa upande wake, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban, alisema kuwa wizara yake imejidhatiti kuweka mazingira bora kwa biashara, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa maabara za kupima viwango vya bidhaa, viwanda, barabara, na viwanja vya ndege.
“Lengo letu ni kuhakikisha biashara na viwanda vinakua kwa kasi kwa kuweka miundombinu imara itakayorahisisha ufanisi na kuongeza mapato,” alisema Waziri Shaaban.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS), Yussuph Majid Nassor, alieleza kuwa mfumo huo umeandaliwa kwa zaidi ya miaka miwili kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo wakiongozwa na TMA.
“Baada ya kupata ithibati kutoka Wakala wa Serikali Mtandao (e-GAZ), leo tunazindua rasmi mfumo huu ambao utaondoa upotevu wa mapato na kurahisisha huduma kwa wadau wetu, kwani sasa hawatalazimika kufika ofisini,” alisema Nassor.
Aliongeza kuwa mfumo huo utawarahisishia wafanyabiashara kufanya malipo ya kibenki kwa wakati wowote, kuondoa matumizi ya nyaraka za kimakaratasi, na kuwapa fursa ya kutoa maoni kwa njia ya mtandao bila kulazimika kuonana ana kwa ana na watumishi wa ZBS.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa e-GAZ, Dk. Said Seif Said, alisema kuwa mabadiliko ya kidijitali yanagusa nyanja zote za maisha na mfumo huo utarahisisha utendaji kazi, kupunguza gharama kwa wafanyabiashara, na kuimarisha uwazi wa huduma za ZBS.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa TMA Kanda ya Afrika Mashariki, Monica Hangi, alisema kuwa ushirikiano wao na ZBS unalenga kuboresha mazingira ya biashara Zanzibar na Afrika kwa ujumla.
“Tuna mashirikiano na nchi 14 za Afrika ili kuimarisha ushindani wa kibiashara, na Zanzibar ni sehemu ya mpango huo,” alisema Hangi.
Aidha, alieleza kuwa mfumo huo utapunguza gharama za upatikanaji wa alama ya ubora kwa zaidi ya asilimia 30, huku shilingi bilioni tatu zikitumika kufanikisha mradi huo, fedha zilizotolewa na washirika wa maendeleo kutoka Norway, Ireland, na Uingereza.