Ujumbe wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) umefanya kikao maalum na Wizara ya Maji pamoja na taasisi zake jijini Dodoma ili kuandaa andiko la mradi wa kusafirisha maji kutoka Bwawa la Farkwa linalojengwa hadi Jiji la Dodoma na Wilaya za Bahi na Chamwino.
Kikao hicho kimehusisha wataalamu kutoka Wizara ya Maji, Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) na Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF), pamoja na kuandaa andiko kikao hicho kimehusu kuweka mikakati ya kufanikisha utekelezaji wa program ya kuendeleza huduma ya majisafi na usafi wa mazingira jijini Dodoma (Dodoma Resilient and Sustainable Water Development and Sanitation Program, DRSWDSP) Awamu ya Pili.
Serikali inashirikiana na AfDB kwa kutekeleza awamu ya kwanza ya programu hiyo (DRSWDSP Phase I), inayojumuisha ujenzi wa Bwawa la Farkwa katika Wilaya ya Chemba ambapo benki hiyo iliipatia Serikali mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani milioni 125.3 kwa ujenzi wa Mtambo wa Kutibu Maji.
Katika hatua nyingine, Serikali imeanza maandalizi ya awamu ya pili ya programu ya DRSWDSP, ambayo inajumuisha ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha maji kutoka Bwawa la Farkwa hadi Jiji la Dodoma pamoja na Wilaya za Bahi na Chamwino.
Kikao kilichofanyika ni cha kwanza kati ya vikao kadhaa vinavyohusisha wadau wa sekta mbalimbali, ikiwemo Wizara ya Maji, Wizara ya Fedha, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, pamoja na taasisi nyingine za Serikali.
Vikao hivi vinatarajiwa kufanyika kuanzia Februari 17 – 28, 2025 lengo likiwa kuandaa andiko la mradi litakalowasilishwa benki ya AfDB mwezi Septemba 2025 ili kupata kibali cha ufadhili.
Hatua hii imefuatia nia ya Benki ya AfDB kufadhili awamu ya pili ya DRSWDSP .