Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi pamoja na wageni mbalimbali kabla ya kuzindua Tume ya Rais ya Kutathmini kuhusu masuala ya mgogoro wa ardhi ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na Tume ya Rais ya Kutathmini zoezi la uhamaji wa hiari wa wakazi wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 20 Februari, 2025.
………………….
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua Tume ya Rais ya Kutathmini kuhusu Masuala ya Mgogoro wa Ardhi katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na Tume ya Rais ya Kutathmini Zoezi la Uhamaji wa Hiari wa Wakazi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Bi. Sharifa Nyanga imesema Uzinduzi wa Tume hizo mbili umefanyika Ikulu Magogoni ikiwa ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Rais Dkt. Samia tarehe 01 Disemba 2024 Mkoani Arusha alipokukutana na kuzungumza na viongozi na wawakilishi wa wananchi wanaoshi eneo la Ngorongoro na maeneo jirani.
Tume hizo mbili zitaongozwa na Mhe. Jaji Dkt. Gerald Ndika ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Kutathmini kuhusu Masuala ya Mgogoro wa Ardhi katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na Mhandisi Musa Iyombe ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Kutathmini Zoezi la Uhamaji wa Hiari wa Wakazi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Aidha, Tume hizo mbili zinajumuisha uwakilishi wa wananchi wanaoishi katika eneo la Ngorongoro na zinatarajia kufanya kazi kwa kipindi cha miezi mitatu.
Pamoja na mambo mengine, wakati wa uzinduzi wa Tume hizo mbili, Rais Dkt Samia ameeleza imani yake kuwa kazi itakayofanywa na Tume hizo itawezesha kupatikana kwa suluhu ya kudumu ya changamoto zilizowasilishwa kwake na viongozi na wawakilishi wa wananchi wanaoishi kwenye eneo la Ngorongoro.
Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizindua Tume ya Rais ya Kutathmini kuhusu masuala ya mgogoro wa ardhi ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na Tume ya Rais ya Kutathmini zoezi la uhamaji wa hiari wa wakazi wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 20 Februari, 2025.