Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya Dkt. Ona Machangu akizungumza na baadhi ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii Wilayani Biharamulo katika ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo katika kukabiliana na ugonjwa wa Marburg.
Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya Dkt. Ona Machangu akiwa katika picha ya pamoja na Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii Wilayani Biharamulo katika ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo katika kukabiliana na ugonjwa wa Marburg.
Na. Elimu ya Afya kwa Umma.
Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya Dkt. Ona Machangu amesema Serikali inatambua Kazi kubwa zinazofanywa na Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kutoa elimu ya Afya nyumba kwa nyumba.
Dkt. Machangu amebainisha hayo katika ufunguzi wa mafunzo ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHWs) ya namna ya kukabiliana na ugonjwa wa Marburg Kata ya Kaniha Wilayani Biharamulo Mkoani Kagera.
Aidha, Dkt. Machangu ametoa wito kwa Wahudumu hao kuendelea kutembelea nyumba kwa nyumba kutoa elimu na hamasa ya kujikinga na ugonjwa wa Marburg ikiwemo unawaji mikono kwa maji tiririka na sabuni kwani hatua hiyo ni muhimu katika kukabiliana na ugonjwa huo pamoja na magonjwa mengine yatokanayo na uchafu.
“CHW ni Nguzo muhimu katika kupambana na ugonjwa wa Marburg ndio maana tumeshiriki mafunzo ya namna ya kuweza kuelimisha na kuhamasisha jamii jinsi wanavyoweza kujikinga na ugonjwa wa Marburg, tunawategemea sana kuweza kufikia nyumba kwa nyumba na kuikoa jamii nzima”, amesema Dkt. Ona
Naye Dkt. Norman Jonas, Mratibu wa Mpango wa Taifa wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii kutoka Wizara ya Afya amesema wahudumu wa afya ngazi ya jamii wamesaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na ugonjwa wa Marburg kwani wamefanya kazi kubwa ya kutoa elimu na hamasa na hata hivyo kupitia mafunzo hayo yatawaongezea uwezo zaidi na kuweza kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.