Mhandisi wa kiwanda cha Mbasira Food Industry akifafanua jambo kwa Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa TIC Dkt. Belineth Mahenge namna kiwanda hicho kinavyofanya uchakataji wa mazao.
Baadhi ya watendaji wa kiwanda cha Mbasira Food Industry wakimweleza mwenyekiti wa TIC changamoto wanazopitia
Mkurugenzi wa Mbasira Food Industry wakati akimwekeza jambo Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa TIC Dkt Belineth Mahenge
Na Neema Mtuka, Sumbawanga
Mkurugenzi wa Mbasira Food Industries Ltd, Sylivery Buyaga, ameiomba Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kusaidia juhudi za kurejesha kiasi cha USD 61,000 kutoka kwa Jeshi la Wananchi wa Sudan.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Sumbawanga, Buyaga alisema kampuni yake iliingia mkataba wa kuuza bidhaa kama unga, mchele, maharage, sukari, mafuta ya kupikia, dengu, na chumvi kwa jeshi hilo. Hata hivyo, biashara hiyo haikukamilika, na kiasi hicho cha fedha hakijarejeshwa licha ya juhudi mbalimbali, ikiwemo barua kwa Balozi wa Sudan nchini Tanzania na Wizara ya Mambo ya Nje bila mafanikio.
Buyaga pia alieleza changamoto nyingine zinazoikumba kampuni hiyo, ikiwemo tozo nyingi za ushuru na ukosefu wa mtaji wa uendeshaji. Alizitaka taasisi kama OSHA, NEMC, TBS, BRELA, na zingine kuweka utaratibu wa ada moja ya kila mwaka badala ya ada nyingi zinazokwamisha uzalishaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TIC, Benelith Mahenge, aliahidi kushughulikia changamoto hizo kwa kushirikiana na serikali ya mkoa na Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuhakikisha mazingira bora kwa wawekezaji wa ndani. Mahenge alisema kuwa sheria mpya ya uwekezaji ya mwaka 2022 inalenga kuwawezesha zaidi wawekezaji wa Kitanzania kunufaika na fursa zilizopo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere, alisisitiza umuhimu wa uwekezaji katika sekta ya viwanda ili kuchangia mahitaji ya ndani ya nchi na kupunguza utegemezi kutoka nje.
Kwa upande mwingine, TIC pia ilitembelea miradi mingine mkoani humo, ikiwemo kiwanda kipya cha juisi na soda cha Dew Drop kinachotarajiwa kuanza uzalishaji Agosti mwaka huu, kikigharimu zaidi ya Shilingi bilioni 50.