Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mkoa wa Lindi Mhe. Mohamed Nyundo amewaasa Wafanyabiashara na Wananchi wa Kilwa kuacha kujihusisha na biashara za magendo kwani zina athari mbaya kwa jamii na uchumi wa nchi.
Mhe. Nyundo ameyasema hayo leo tarehe 10.02.2025 wakati alipotembelewa na Timu ya Maafisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) waliofika ofisini kwake kwa lengo la kujitambulisha kabla ya kuanza zoezi la kutoa elimu ya kodi mlango kwa mlango wilayani hapo.
Mhe. Nyundo ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.
Naye, Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Lindi Bw. Faraji Mkikima amefafanua kuwa, TRA itaendelea kusimamia sheria ikiwa ni pamoja na kutoa elimu juu ya madhara ya biashara hiyo ili kuondoa vitendo hivyo vya watu kujihusisha na biashara za magendo.
Timu ya Maafisa wanaotoa elimu ya mlango kwa mlango wilayani hapo, imefanikiwa kufanya semina ya kodi kwa Wafanyabiashara ambayo imefunguliwa na Mkuu wa Wilaya wa Kilwa Kivinje na pia imewatembelea walipakodi katika maeneo yao biashara na kuwaelimisha masuala mbalimbali yanayohusu kodi.