ILANI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imetoa maelekezo kwa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kutekeleza miradi mbalimbali kwa lengo la kuboresha maendeleo ya wananchi wake.
Ziara ya siku nne ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kwenye Visiwa vya Unguja na Pemba kuanzia tarehe 17 hadi 20 Januari, 2020 ilikuwa na lengo la kuhakikisha ilani inatekelezwa kwa vitendo.
Ziara hiyo ambayo ililenga kufuatilia utekelezaji wa maelekezo ya Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015 – 2020 ni sehemu ya utaratibu wa kawaida wa Waziri Mkuu kutembelea mikoa yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri Mkuu alikagua shughuli mbalimbali hususan utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mikoa ya Kusini Unguja, Mjini Magharibi na Kaskazini Unguja. Kwa upande wa Pemba alitembelea miradi mbalimbali ya maendeleo katika mikoa ya Kusini Pemba na Kaskazini Pemba.
Mbali na kuzungumza na watumishi, kusalimia wananchi pamoja na kupata mrejesho kuhusu kero na malalamiko yao, pia Waziri Mkuu, alisisitiza umuhimu wa watumishi wa umma kufuatilia makusanyo ya mapato na kudhibiti matumizi ya fedha za walipa kodi.
MAPATO
Katika Suala la mapato, Waziri Mkuu alisisitiza kuwa Serikali zote mbili (SMT na SMZ) zipo makini na matumizi ya fedha zinazotokana na kodi za wananchi, hivyo mtumishi yeyote atakayebainika kujihusisha na ubadhirifu wa mapato ya Serikali hatoonewa haya.
Waziri Mkuu alisema ili Taifa lolote liweze kupata maendeleo ni vema matumizi sahihi ya fedha za walipa kodi yakasimamiwa ipasavyo. Alisisitiza kuwa viongozi hawanabudi kutambua kuwa Serikali zote mbili za Muungano na Zanzibar zipo makini na matumizi ya fedha hizo.
Aidha, akiwa katika mkoa wa Kusini Unguja, Waziri Mkuu aliwaagiza wakuu wote wa mikoa na wilaya wahakikishe wanachukua hatua kali kwa watumishi wa umma ambao hawatekelezi majukumu yao ipasavyo, pamoja na watakaobainika kufanya ubadhirifu wa fedha za umma.
Pia aliwataka watumishi wa umma wasimamie vizuri ukusanyaji wa mapato na wahakikishe fedha zote zinazopatikana zinaingizwa kwenye mfuko wa Serikali. “Ni muhimu kwa watumishi kushirikiana katika ukusanyaji wa mapato ili Serikali iweze kupata fedha za kugharamia miradi ya maendeleo.”
Alisema ni vema wakasimamia makadirio ya ukusanyaji wa mapato na wahakikishe wanabaini vyanzo vyote na wafuatilie iwapo makadirio hayo ni sahihi na fedha zote zinazokusanywa kama zinaingia katika mfuko mkuu wa Serikali. Aliongeza kuwa makusanyo yafanyike kielektroniki.
KIWANDA CHA SUKARI CHA ZANZIBAR
Waziri Mkuu alitembelea Kiwanda cha Sukari cha Zanzibar kilichopo eneo la Mahonda kwa lengo la kujionea shughuli za uzalishaji kiwandani hapo, ambapo alipokea malalamiko ya kukosekana kwa soko la sukari inayozalishwa kiwandani hapo na ardhi ya kutosha kuongeza kilimo cha miwa kutoka kwa mwekezaji Bw. Rahim Bhaloo.
Mwekezaji huyo, alidai kuwa licha ya mahitaji ya tani 36,000 za sukari kwa upande wa Zanzibar, anashindwa kupata soko la tani 6,000 anazozalisha kiwandani hapo, ambapo Waziri Mkuu alimwelekeza Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar kuratibu vizuri utoaji wa vibali vya sukari kutoka nje ili kuhakikisha sukari yote inayozalishwa na mwekezaji inanunuliwa.
Waziri Mkuu, alisisitiza umuhimu wa kulinda wawekezaji wa ndani na akasisitiza kuhusu kufanya kazi pamoja baina ya Serikali na muwekezaji ili kukuza ajira na soko la huduma.
Alimtaka Mkuu wa mkoa Kaskazini Unguja, kuhamasisha wananchi kulima miwa kwa kuwa soko la uhakika lipo na Halmashauri ya Wilaya ya Kati ione uwezekano wa kupata ardhi kwa ajili ya mwekezaji kuongeza uzalishaji.
“Wizara ya Viwanda lazima mbadilike na muweke utaratibu mzuri wa kusimamia uingizwaji wa sukari kutoka nje. Haiwezekani sukari inayozalishwa ndani ikakosa soko kutokana na uingizwaji wa sukari kutoka nje. Hatuwezi kumfurahisha mtu mmoja huku wengi wakiumia.”
Waziri Mkuu alisema Serikali imeamua kukuza uchumi kwa kupitia sekta ya viwanda hivyo ni lazima viwanda vya ndani vikalindwa. “Viwanda vinasaidia katika kuondoa tatizo la ajira, vinawapa wakulima soko la uhakika la mazao yao pamoja na Serikali kupata kodi ya uhakika.”
Waziri Mkuu alisema “haiwezekani sukari inayotengezwa na kiwanda hicho ambayo ubora wake umethibitishwa na Shirika la Viwango Zanzibar ikakosa soko hii haiwezekani tukashindwa kununua tani 6,000 huku mahitaji yetu ni tani 36,000.”
Alisema sera ya nchi inasisitiza umuhimu wa kulinda wazalishaji wa ndani ambao bidhaa zao zimethibitishwa na mamlaka husika. Hivyo, ni lazima kuwalinda wawekezaji kwa kuhakikisha wanapata masoko ya uhakika pamoja na kuhamasisha wananchi kutumia bidhaa hizo.
Awali,Mkurugenzi Mkaazi wa kiwanda cha Sukari Zanzibar, Bw. Rahim Bhaloo alisema kiwanda chao kinazalisha tani 6,000 kwa mwaka huku kikiwa na uwezo wa kuzalisha tani zaidi ya 20,000 kwa mwaka ila tatizo ni soko pamoja na ardhi ya kutosha kulima miwa.
Alisema kutokana na uhaba wa soko sukari waliyozalisha katika msimu wa mwaka 2019/2020 wameuza tani 2,800 tu na kiasi cha tani 3,200 bado kipo kiwandani hapo, hivyo ameiomba Serikali iwasaidie kwa kuwatafutia masoko pamoja na ardhi ili waweze kuongeza uzalishaji.
Mkurugenzi huyo aliiomba Serika iwe inazuia utoaji wa vibali vya uagizaji wa sukari kutoka nje hususani kipindi cha uzalishaji ili waweze kuuza sukari yao na itakapoisha ndio vibali hivyo vianze kutolewa. Kiwanda kimeajiri wafanyakazi 300, pia wakulima wa nje zaidi ya 800 wanauza miwa yao kiwandani hapo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar, Bw. Juma Hassan Reli amemhakikishia Waziri Mkuu kwamba sukari yote iliyopo kiwandani hapo itakuwa imeshanunuliwa ifikapo Februari mwaka huu. Pia maelekezo yote aliyoyatoa kuhusu utoaji wa vibali vya uagizaji wa sukari watayafanyia kazi.
AFYA
Waziri Mkuu alitembelea Kituo cha Afya cha Kizimkazi, Dimbani kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya Kusini ambayo ilikuwa ni siku ya Afya ya Kijiji, ambapo alizindua mashine ya ultra sound, kukagua huduma za afya zilizokuwa zikitolewa ikiwemo upimaji wa afya kwa magonjwa ya shinikizo la damu, meno, macho, uzito pamoja na homa ya ini. Vilevile, aligawa vyandarua kwa akina mama wawili wajawazito kwa niaba ya wenzao 10.
Waziri Mkuu aliwataka wajawazito aliowakabidhi vyandarua pamoja na wananchi wengine wavitumie kujikinga na mbu na si kwa matumizi mengine tofauti kwa kuwa Serikali imegharamia vyandarua hivyo kwa fedha nyingi.
Pia, Waziri Mkuu alizindua jengo la huduma ya mama na mtoto (yaani Kituo cha Uzazi – Bambi) kilichopo katika Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua mbalimbali ilizochukua katika kuboresha huduma za afya.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi watumie vituo vyote vya afya kwa ajili ya kupima na kutambua afya zao. Aliongeza kuwa ujenzi wa kituo hicho ni sehemu ya jitihada kubwa inayofanywa na Serikali zote mbili kwa lengo la kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Waziri Mkuu amewataka watumishi wa Sekta ya Afya waimarishe utoaji wa huduma hizo kwa wananchi kwa sababu Serikali imefanya mabadiliko kwenye sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti ya dawa. Katika kukabiliana na uchache wa watumishi katika Sekta ya Afya, Serikali ya SMZ tayari imeajiri watumishi wapya 150 hivi karibuni.
ELIMU
Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa Kituo cha Mafunzo ya masomo ya Sayansi kilichopo katika Jimbo la Paje-Unguja ambapo alisema ameridhishwa na ujenzi wa mradi huo ambapo utakapokamilika utasaidia katika kupunguza changamoto ya walimu wa kufundisha masomo ya sayansi.
Alisema kuwa walimu wa masomo ya sayansi ni changamoto kubwa nchi nzima, hivyo, Serikali zote mbili zinaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kukabiliana na tatizo hilo. Hatua hizo ni pamoja na ujenzi wa vituo vya aina hiyo 22 kwa upande wa SMZ.
“Mkakati wa kuboresha mafunzo ya sayansi ni sehemu ya kupata wataalamu kwa ajili ya kuifikia ndoto ya Tanzania ya uchumi wa viwanda, hivyo alimtaka Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ahakikishe ujenzi huo unakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa ifikapo tarehe 31 Machi 2020.
Akiwa kisiwani Pemba Waziri Mkuu alikagua maendeleo ya ujenzi wa chuo cha Mafunzo ya Amali cha Daya kilichopo Mtambwe wilaya ya Wete, Kaskazini Pemba, ambapo aliwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini wasimamie ipasavyo suala la elimu hususani kwa watoto wa kike.
“Hakikisheni elimu kwa mtoto wa kike inasimamiwa vizuri na kuchukua hatua kwa watakaowakatisha masomo.Pia, Waziri Mkuu aliwataka Watoto wa kike watoe taarifa za watu wanaotaka kuwakatisha masomo yao kwa viongozi wa shehiya (vijiji) waliopo kwenye maeneo yao.
Waziri Mkuu alisema Serikali imedhamiria kuwalinda watoto wa kike lengo likiwa ni kuhakikisha wanamaliza masomo yao na hatimaye waweze kujikwamua wao pamoja na familia zao. “Wanafunzi wa kike hakikisha mtu yeyote atakayekugusa, kukufuatilia nenda kamshtaki kwa kiongozi wa Shehiya husika. Vijana jihadharini na watoto wa shule ukikutwa naye jela miaka 30.”
Akizungumzia kuhusu taarifa za ufaulu hali ya ufaulu, Waziri Mkuu alionesha kutoridhishwa kwa Kiwango cha ufaulu hususan wa Elimu ya msingi, hivyo, ameuagiza uongozi wa Wizara ya Elimu uhakikishe unafanya mabadiliko katika kuisimamia sekta hiyo. “Maafisa elimu waache kukaa maofisini waende mashuleni kusimamia ufundishaji.”
Alisema Serikali inataka kuona watoto wakifanya vizuri kuanzia ngazi ya elimu ya msingi hadi elimu ya juu. “Ili malengo hayo yatimie ni lazima watendaji katika sekta ya elimu wakabadilika na kusimamia vizuri ufundishwaji. Tunataka watoto wanapoanza masomo yao ya msingi wafike hadi ngazi ya chuo kikuu ili tuwe na wataalamu wengi.”
Pia Waziri Mkuu alitembelea Chuo cha kilimo cha Kizimbani ambacho kimepandishwa hadhi na kuwa chuo kikuu kishiriki cha SUZA. Hata hivyo uongozi wa chuo hicho ulimueleza kwamba chuo kinakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa hati ya umiliki wa eneo la Makuyuni lililopo Bagamoyo ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ililitoa kwa Chuo cha Kilimo cha Kizimbani.
Akizungumza na wanafunzi na wananchi chuoni hapo Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa kujifunza kwa bidii na kujenga dhana ya kujiajiri hususan katika kilimo badala ya kutegemea ajira chache zinazotoka Serikalini. Pia, Waziri Mkuu aliiagiza Wizara ya Kilimo na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar zishirikiane na wenzao wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumaliza changamoto ya umiliki wa eneo la Makuyuni, Bagamoyo.
“Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ishirikiane na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutatua changamoto ya wahadhiri chuoni hapa na Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar atenge bajeti kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya chuo sambamba na kununua matrekta kwa ajili ya mafunzo ya amali.”
Kadhalika, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Mwera samabamba na kukagua chanzo cha maji na nishati ya umeme wa jua itakayotumika kuendesha mradi huo, ambapo alimpongeza mwakilishi wa jimbo la Mwera, Mheshimiwa Mihayo kwa kuchangia ujenzi wa mradi huo.
Akiongea na wananchi wa Mwera, Waziri Mkuu alielekeza kuwa Halmashauri ziunge mkono juhudi hizo kwa kutafuta fedha za kukamilisha mradi na kuibua miradi mingine. Mradi huo unahusisha ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji pamoja na usambazaji kwa wananchi.