Na Mwandishi wetu Mihambwe
Afisa Tarafa Mihambwe, Emmanuel Shilatu amekea vikali tabia ya uzembe na mivutano inayosababisha kusua sua ujenzi wa miradi ya kimaendeleo kwani haina tija kwa jamii.
Gavana Shilatu ameyasema hayo alipotembelea Shule ya Msingi Namunda iliyopo kata ya Kitama na kukuta ujenzi wa choo tundu 9 haujaanza kutokana na uzembe licha ya kuwepo kwa vifaa na fedha kujengea na hivyo kutoa saa 24 ujenzi uanze mara moja.
“Hapa tofali zipo, mchanga upo, saruji ipo, fedha ipo, ramani ipo, nguvu kazi ipo lakini ajabu yake hadi sasa ujenzi wa vyoo tundu tisa bado haujaanza. Ni uzembe wa hali ya juu usiokubalika, naukemea kwa nguvu zote. Ndani ya saa 24 nataka zoezi la uchimbaji shimo liwe limeanza na ujenzi uendelee. Kama kawaida yangu kesho nitakuja kukagua utekelezaji wa agizo langu.” alisema Gavana Shilatu.
Katika ziara hiyo Gavana Shilatu aliambatana na Mwenyekiti wa Kijiji, Mtendaji Kijiji, Wajumbe Kamati ya ujenzi na kupokelewa na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ya Namunda na Kamati ya shule.