Kutoka kushoto ni Rais William Ruto wa Kenya, ambaye ni Mwenyekiti wa EAC, na Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe, Mwenyekiti wa SADC, kulia ni Elias Masisi Katibu Mtendaji wa SADC.
………………
NA JOHN BUKUKU- IKULU MAGOGONI
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimeazimia kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha mapigano yanayoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) yanakomeshwa mara moja. Katika azimio lao, viongozi wa jumuiya hizi wamesisitiza umuhimu wa kutumia mbinu za kidiplomasia, kijeshi, na kibinadamu ili kurejesha amani na utulivu nchini humo.
Mkutano huo pia umetoa maagizo maalum kwa wakuu wa majeshi wa EAC na SADC kukutana ndani ya siku tano ili kutoa mwelekeo wa kiufundi kuhusu utekelezaji wa hatua za kusitisha mapigano bila masharti. Wakuu hao wa majeshi wametakiwa kuandaa mpango wa dharura wa msaada wa kibinadamu unaojumuisha urejeshaji wa miili ya marehemu, uokoaji wa majeruhi, na kuhakikisha utoaji wa misaada kwa waathirika wa vita.
Aidha, mpango huo unalenga pia kuimarisha usalama katika Goma na maeneo jirani, kufungua njia kuu za usambazaji kama vile Goma-Sake-Bukavu, Goma-Kibumba-Rumagambo-Kalegera, Rutsuru-Bunagana, na Goma-Kiwanja-Rwindi-Kanyabayonga-Nyonga-Lubero. Pia, wakuu wa majeshi wameagizwa kuimarisha usafiri wa majini katika Ziwa Kivu kati ya Goma na Bukavu, kufungua uwanja wa ndege wa Goma mara moja, na kutoa mapendekezo ya hatua nyingine muhimu za usalama.
Maazimio haya yanaweka msingi wa matumaini ya kukomesha vita vya takribani miongo mitatu vinavyoikumba Congo DRC. Ikiwa hatua hizo zitatekelezwa ipasavyo, raia wa DRC watapata nafasi ya kuishi kwa amani na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Maazimio hayo yametolewa baada ya mkutano wa pamoja wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika tarehe 8 Februari 2025, jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kanda, wakiwemo Rais William Ruto wa Kenya, ambaye ni Mwenyekiti wa EAC, na Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe, Mwenyekiti wa SADC. Pia, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya (SADC-Organ) ambaye alihudhuria kama mwenyeji wa mkutano huo.
Viongozi wengine waliokuwepo ni Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Rais Hakainde Hichilema wa Zambia, Rais Hassan Sheikh Mohamed wa Somalia, pamoja na wawakilishi kutoka mataifa ya Angola, Botswana, Congo DRC, Malawi, Mauritania, Burundi, South Sudan, na Msumbiji.
Viongozi hawa walijadili hali ya usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kutoa maazimio ya pamoja ya kusitisha mapigano na kurejesha amani katika eneo hilo.
Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Rais Samia Suluhu Hassan Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya (SADC-Organ)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya mapoja na Marais wenzake na baadhi ya viongozi wa juu waserikali za nchi za SADC na EAC.