Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Rais wa Rwanda Paul Kagame wakati alipowasili kwa ajili ya kushiriki mkutano wa Pamoja wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika tarehe 08 February 2025 Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa EAC, Rais wa Kenya Dk. William Ruto,
………………
Jiji la Dar es Salaam limeandaa mkutano muhimu uliowakutanisha Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kwa lengo la kujadili suluhu ya kidiplomasia kwa mgogoro wa muda mrefu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mwenyekiti wa EAC, Rais wa Kenya Dk. William Ruto, alisisitiza kuwa amani ya kudumu DRC inaweza kupatikana kupitia njia za mazungumzo badala ya matumizi ya nguvu za kijeshi.
“Historia ya DRC imejaa changamoto za muda mrefu. Huu ndio wakati wa viongozi kuchukua hatua madhubuti. Mazungumzo ya kidiplomasia ni suluhisho bora kuhakikisha umoja na amani ya kudumu nchini humo,” alisema Rais Ruto wakati wa hotuba yake ya ufunguzi iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Rais Ruto alieleza kuwa vita vya DRC vimesababisha madhara makubwa kwa wananchi, ikiwemo mamilioni ya watu kuhama makazi yao, watoto kushirikishwa katika makundi ya waasi, na kuzorota kwa shughuli za uzalishaji mali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa SADC na Rais wa Zimbabwe, Dk. Emerson Mnangagwa, alitoa wito wa mshikamano miongoni mwa nchi za Afrika, akilinganisha changamoto za DRC na harakati za ukombozi wa bara hilo.
“Mgogoro wa DRC unapaswa kuwaunganisha Waafrika kama ilivyokuwa wakati wa harakati za uhuru. Umoja wetu ni muhimu katika kuhakikisha usalama na ustawi wa wananchi wa nchi hiyo,” alisema Rais Mnangagwa.
Mwenyeji wa mkutano huo, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, alieleza kuwa ni jukumu la viongozi wa EAC na SADC kuhakikisha mgogoro huo unamalizika kwa manufaa ya wananchi wa DRC.
“Wananchi wa DRC wanateseka. Wameshindwa kushiriki shughuli za kijamii na kiuchumi kwa muda mrefu. Huu ni wakati wa kufungua ukurasa mpya wa amani na ustawi wa wananchi hao,” alisema Rais Samia.
Mkutano huo, ambao pia ulihudhuriwa na viongozi kama Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, na Rais Hakainde Hichilema wa Zambia, ulilenga kutafuta mbinu shirikishi kwa kushirikiana na wadau wa kimataifa na mashirika ya kiraia kuleta amani ya kudumu DRC.
Viongozi hao waliweka bayana kuwa ushirikiano wa kanda hizo mbili ni muhimu katika kuhakikisha mzozo wa DRC unashughulikiwa kikamilifu kwa kutumia njia za kidiplomasia.