Mhe. Veronika Mueni Nduva Katibu mtendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki akizungumza katika kikao hicho cha Mawaziri wa Mambo ya nje na ulinzi kutoka nchi za EAC na SADC.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akizungumza katika kikao hicho.
Mhe. Elias Magosi Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC akizungumza katika kikao hicho cha mawaziri.
………………
NA JOHN BUKUKU-IKULU MAGOGONI
Jijini Dar es Salaam, Mawaziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamekutana leo, Februari 7, 2025, katika jitihada za kuimarisha mshikamano wa kikanda kwa kutafuta suluhu ya mzozo unaoendelea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Kikao hicho kinafungua njia ya mkutano wa marais wa jumuiya hizo utakaofanyika kesho jijini humo.
Kwa kushirikiana na viongozi wa ngazi ya juu wa EAC na SADC, kikao hicho kiliongozwa na Katibu Mkuu wa EAC, Mhe. Veronika Mueni Nduva, na Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Elias Magosi. Mawaziri walioongoza kikao hicho walikuwa Mhe. Musalia Mudavadi wa Kenya na Prof. Amon Murwira wa Zimbabwe.
Akihutubia kikao hicho, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, alisisitiza umuhimu wa mshikamano wa kikanda na kupongeza juhudi za viongozi wa EAC na SADC katika kushughulikia mgogoro wa DRC. Alimshukuru Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kihistoria.
“Ni matumaini yangu kikao hiki kitaandaa njia bora kwa kikao cha marais wa kesho, na hatimaye kupatikana kwa amani ya kudumu nchini Congo. Nawashukuru wote kwa juhudi zenu,” alisema Balozi Kombo.
Kwa upande wake, Mhe. Veronika Mueni Nduva alisisitiza kuwa usalama wa DRC ni muhimu si kwa nchi hiyo pekee, bali kwa ustawi wa kikanda. “Tunapaswa kusimama pamoja kuhakikisha hali hii ya mgogoro inashughulikiwa kwa umoja na mshikamano,” alisema.
Naye Mhe. Elias Magosi wa SADC aliweka msisitizo juu ya dharura ya kuchukua hatua za haraka. “Vita hii imegharimu maisha ya wengi na kuleta mateso makubwa kwa wanawake na watoto. Ni lazima wahusika wa mgogoro huu wakomeshe mapigano na kushiriki mazungumzo ya amani,” alisema.
Mkutano huu unatarajiwa kutoa mapendekezo ya msingi yatakayojadiliwa na Wakuu wa Nchi wa EAC na SADC kesho, huku lengo likiwa ni kuimarisha amani, usalama, na mshikamano wa kikanda kwa manufaa ya wananchi wa DRC na ukanda mzima.