Jumoke Jagun-Dokunmu, mkurugenzi wa IFC kanda ya Afrika Masharikia akizungumza katika hafla ya makubaliano ya ubia kati ya IFC na TMRC kwa ajili ya kuwekeza kwa muda mrefu kiasi cha dola za marekani milioni 5.75 fedha za Tanzania ambazo ni Shilingi bilioni 13.3 kwa ajili ya kuwezesha ukuaji wa soko la mikopo ya nyumba za makazi Tanzania uliofanyika kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es salaam leo jijini Dar es salaam leo.
Bw. Charles Itembe Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakrugenzi ya TMRC akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es salaamleo.
Mkurugenzi wa Uchumi, Utafiti na Sera wa BoT, Suleiman Misango akielezea jinsi Benki Kuu ya Tanzania inavyoshirikiana na taasisi za kimataifa katika kukuza sekta mbalimbali za kiuchumi hapa nchini Tanzania.
Bw. Oscar Mgaya Mkuregenzi Mtendaji wa TMRC akitoa maelezo jinsi taasisi hiyo ya kusaidia mabenki katika uwekezaji wa mikopo ya ujenzi wa nyumba katika hafla iliyofanyika kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es salaam leo.
Jumoke Jagun-Dokunmu, mkurugenzi wa IFC kanda ya Afrika Mashariki kulia na Bw. Charles Itembe Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakrugenzi ya TMRC wakipongezana mara baada ya kutangaza rasmi makubaliano hayo.
Picha ya pamoja.
……………………………………………………..
Benki ya Dunia kupitia shirika lake la fedha (IFC), ambalo ni mojawapo ya taasisi za benki ya dunia leo inatangaza kuwa imeingia ubia na TMRC kwa kuwekeza kwa muda mrefu kiasi cha dola za marekiani milioni 5.75 kwa fedha ya Tanzania ambazo ni Shilingi bilioni 13.3 kwa ajili ya kuwezesha ukuaji wa soko la mikopo ya nyumba za makazi Tanzania na pia kuwezesha upatikanaji wa nyumba za makazi za gharama nafuu.
Uwekezaji huo unahusisha shirika hilo la IFC kununua hisa za TMRC zenye thamani ya dola za Marekani milioni 1.5 ambazo zimelipiwa kwa shilingi za kitanzania na pia kuwekeza kiasi cha dola za Marekani milioni 4.25 zitakazotolewa ambazo zitatumika kuwezesha TMRC kutoa hatifungani zake kwenye soko la mitaji la Tanzania kwa muda wa miaka mitano. Uwekezaji huu wa IFC umewezeshwa na dirisha la sekta binafsi linalotumia fedha zilizotengewa/idhinishwa kwa nchi husika kwa ajili ya uwekezaji.
Jumoke Jagun-Dokunmu, mkurugenzi wa IFC kanda ya Afrika Mashariki alisema kuwa IFC imejipanga kuwezesha ukuaji wa soko la nyumba hapa Afrika kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za ndani za muda mrefu ambazo ni muhimu kwa ukuaji wa masoko ya nyumba. Kwa IFC kuwekeza TMRC, IFC inategemea kuongeza kasi ya ukuaji wa soko la nyumba za gharama nafuu hapa Tanzania.”
TMRC ni taasisi ya fedha ilianzishwa mwaka 2010 ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa serikali ya Tanzania wa mikopo ya nyumba uliofadhiliwa na benki ya dunia na inasimamiwa na Banki Kuu ya Tanzania kwa niaba ya serikali. Benki ya dunia kupitia Benki Kuu ya Tanzania ilitoa fedha za uendeshaji za awali kiasi cha dola za kimarekani zipatazo milioni 70 kwa ajili ya kuwezesha TMRC kutoa mikopo kwa mabenki kwa ajili ya kuziwezesha kukopesha wateja wake mikopo ya nyumba za makazi kwa muda mrefu. Kupitia mikopo hii ya muda mrefu kwa benki, TMRC imewezesha ukuaji wa soko la mikopo ya nyumba. Idadi ya mikopo ya nyumba iliongezeka kutoka mikopo 579 mwaka 2011 hadi mkopo 5,411 mwaka 2019. Mikopo ya TMRC kwa benki pia imewezesha muda wa mikopo ya nyumba kuongezeka kutoka wastani wa miaka 5 hadi 7 mwaka 2011 na kufikia muda wa juu wa mikopo ya nyumba kama ilivyoruhusiwa kisheria wa miaka 25 na hivyo kuongeza uwezo wa wakopaji kupata mikopo ya nyumba kwa kuwa rejesho la kila mwezi hupungua kutokana na marejesho ya mkopo.
Hadi sasa, TMRC imeshatoa mikupuo miwili ya hatifungani yake yenye thamani ya shilingi bilioni 21.7 na kuiiorodhesha kwenye soko la hisa la Dar es Salaam. Hatifungani ya TMRC imeiwezesha TMRC kupata fedha za uendeshaji kutoka kwenye masoko ya mitaji Tanzania na hivyo kupunguza utegemezi kwa pesa za uma. IFC itashiriki kwenye mikupuo ijayo ikihitajika kuhakikisha kuwa toleo lijalo linafanikiwa kwa kiasi kikubwa na kuiwezesha TMRC kufikia malengo yake.
“Uwekezaji huu wa IFC utaiwezesha TMRC kuvutia wawekezaji wengine wapya kwenye hatifungani yake, na hivyo kuwezesha TMRC kupata fedha za muda mrefu, kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kuendeleza shughuli zake za kuwezesha mabenki kutoa mikopo ya nyumba za makazi kwa wateja wao,” kulingana na maoni ya Bw. Oscar Mgaya, Afisa Mtendaji Mkuu wa TMRC.
Uwekezaji wa IFC kwenye shughuli za TMRC utaambatana na ujengaji uwezo kwenye masoko ya nyumba, utoaji elimu kwa umma kuhusu mikopo ya nyumba, kujenga uwezo wa benki zinazotoa mikopo ya nyumba kuhusu namna bora ya kutoa mikopo ya nyumba, maelezo kuhusu mikopo hiyo, usimamizi wa mikopo ya nyumba na usimamizi wa mikopo na amana za benki.