Mwana wa Mfalme Rahim Al-Hussaini ameteuliwa kuwa Imam wa 50 wa madhehebu ya Ismailia kufuatia kifo cha baba yake, Mtukufu Aga Khan IV, aliyefariki dunia Februari 4, 2025, jijini Lisbon, Ureno.
Rahim ametangazwa kurithi nafasi hiyo baada ya kufunguliwa kwa wosia wa marehemu baba yake.
Kwa zaidi ya miaka 1,400 ya historia yao, waumini wa Ismailia wameongozwa na Imamu wa kizazi cha urithi. Waismailia, ambao idadi yao inakadiriwa kuwa kati ya milioni 12 hadi 15, wanaishi katika zaidi ya nchi 35 duniani.
Mwana wa Mfalme Rahim amekuwa mstari wa mbele kusimamia Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), akijikita zaidi katika kulinda mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi. Yeye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira na Tabianchi, ambapo ameonyesha juhudi kubwa katika kusaidia taasisi za kijamii za Ismailia kukabiliana na changamoto za umasikini, elimu, mafunzo, na ujasiriamali.
Aidha, Mwana wa Mfalme Rahim hukutana mara kwa mara na viongozi wa serikali, mashirika ya kimataifa, na asasi za kiraia ili kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizo na kuendeleza juhudi za AKDN za kuboresha maisha ya jamii zilizo pembezoni na zilizo hatarini zaidi.
Rahim alizaliwa Oktoba 12, 1971, na ni mtoto wa kwanza wa Mwana wa Mfalme Karim Aga Khan na mkewe wa kwanza, Binti Mfalme Salimah. Alipata elimu yake katika Shule ya Phillips Academy Andover na kuhitimu mwaka 1995 katika Chuo Kikuu cha Brown, akitunukiwa Shahada ya Sanaa katika Fasihi Linganishi.
Ana watoto wawili, Mwana wa Mfalme Irfan (aliyezaliwa 2015) na Mwana wa Mfalme Sinan (aliyezaliwa 2017). Rahim pia ni msimamizi wa bodi za mashirika mbalimbali ya AKDN na amekuwa akifuatilia kwa karibu kazi za Taasisi ya Mafunzo ya Ismailia pamoja na taasisi nyingine za kijamii za madhehebu ya Ismailia.