Na WAF – USWISI
Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, leo Februari 5, 2025, amewasilisha mada kuhusu uimarishaji wa mikakati ya Bima ya Afya kwa Wote katika siku ya tatu ya Mkutano wa 156 wa Bodi Tendaji ya Shirika la Afya Duniani (WHO) unaoendelea Geneva nchini Uswisi.
Dkt. Magembe ameanza kwa kuzishukuru Nchi Wanachama kwa kutoa pole kwa familia ya Dkt. Faustine na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi Mteule wa WHO Kanda ya Afrika, Dkt. Faustine Ndugulile.
Amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na WHO katika kutekeleza mikakati yake ya afya kwa lengo la kuboresha huduma za afya kwa wananchi wake na Dunia kwa ujumla.
Akiainisha hatua zinazochukuliwa na Tanzania katika kuimarisha afya kwa wote, Dkt. Magembe amesema nchi imetunga na kuanza utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ili kuwezesha wananchi kupata huduma za afya kwa gharama nafuu.
Aidha, Tanzania imewekeza kwenye huduma za afya ya msingi, ambapo takriban asilimia 70 ya wananchi wanapata huduma hizo ndani ya umbali wa kilomita tano kutoka wanapoishi.
“Tunaendelea kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili waweze kutambua magonjwa kwa haraka na kuimarisha afua za kinga,” amesema Dkt. Magembe na Kuongeza,
“Serikali pia inaendelea kuwekeza katika rasilimali watu, vifaa tiba na teknolojia za kisasa kwa lengo la kuboresha huduma za kibingwa na bobezi, kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zaidi ndani ya nchi,” amefafanua Dkt. Magembe.
Tanzania inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha huduma bora za afya zinawafikia wananchi wote kwa ufanisi, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kufanikisha lengo la afya kwa wote.