Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke, Bw. Ismail Bukuku akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 5, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya utendaji.
……………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imefatilia miradi ya maendeleo 12 yenye thamani ya shilingi 4, 832, 450, 550, huku mradi mmoja wa ujenzi wa jengo la ghorofa tatu katika Shule ya Sekondari Mangaya ulibainika kuwa na mapungufu baada ya mkandarasi kutumia square pipes zenye upana wa 2.3 cm kutengeneza madirisha ya jengo hilo badala ya kutumia 2.5cm kama ilivyoelekezwa katika maelezo ya gharama za kazi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 5, 2025 Jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya utendaji, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke, Bw. Ismail Bukuku, amesema kuwa wamefanya ufuatiliaji kwenye miradi huo wakishirikiana na wataalamu wa Manispaa ya Temeke kuangalia jengo hilo na kubaini limejengwa kwa kiwango kisichokusudiwa na thamani ya fedha (value of Money).
Bw. Bukuku amesema kuwa jengo hilo la ghorofa tatu katika Shule ya Sekondari Mangaya linajengwa kwa thamani ya gharama ya shilingi bilioni 1.6 unaotekelezwa na mkandarasi Mbaza Engineering Company Ltd.
’’Takukuru baada ya kubaini ya mapungu hayo ya vipimo vya Square Pipes tulitoa maelekezo kwa msimamizi wa mradi ambaye ni Ofisi ya Mkurugenzi wa Temeke kupitia Mhandisi wa Manispaa hiyo kuwa Square Pipes zenye upana wa 2.3cm zilizotumika kujenga madirisha ya jengo husika zibadilishwe na badala yake ziwekwe zenye upana wa 2.5 cm kama ilivyoelezwa katika mradi huo” amesema Bw. Bukuku.
Amefafanua kuwa Ofisi ya Manispaa ya Temeke ilimtaka mkandarasi kubadilisha square pipes za madirisha ya jengo husika na kuweka zenye upana kulingana na maelekezo ya thamani ya halisi ya mradi, huku akieleza kuwa Disemba 19, 2024 maafisa wa TAKUKURU walifika katika mradi huo na kujiridhisha kuwa square pipes za madirisha ya jengo hilo na kuona tayari mkandarasi amefanya marekebisho.
Amesema kuwa ni muhimu taasisi zote zinazotekeleza miradi ya maendeleo katika mkoa wa Temeke kuwasimamia vizuri wakandarasi katika kuhakikisha wanatekeleza miradi ya maendeleo kwa kuzingatia maelezo ya gharama za kazi ili kuleta thamani ya fedha za miradi husika na kuepuka madhara yanayoweza kutokea siku za usoni.
Katika hatua nyengine Bw. Bukuku amesema kuwa wamefanikiwa kupokea malalamiko 34 yaliohusu vitendo vya rushwa na kuendelea kufanyiwa uchunguzi ili kuthibitisha tuhuma katika hatua mbalimbali.
Amesema kuwa pia kesi moja ya Jinai namba 202312270000829/2023 Mshtakiwa Bw. Shamte Abdalah Mtumba alikuwa anatuhumiwa kwa kosa la kuomba na kupokea hongo ya Sh. 100,000, Jamhuri imefanikiwa kushinda kesi hiyo baada ya mtuhumiwa kupatikana na hatia na kuhukumiwa kulipa faini ya sh. 500,000 au kwenda jera miaka mitatu, mtuhumiwa alifanikiwa kulipa faini.
’’Tunawapongeza wananchi wa Mkoa wa Temeke na Wilaya ya Kigamboni kwa kuendelea kushiriki katika kuzuia vitendo vya rushwa : Kuzuia Rushwa ni jukumu lako na langu; tutimize wajibu wetu” amesema Bw. Bukuku.
Takukuru Mkoa wa Temeke umejipanga vyema kwa ajili ya mwaka 2025 katika kutekeleza majukumu yao kwa vitendo ikiwemo kuendelea kuimarisha juhudi za kuzuia rushwa kwa kuongeza ushiriki wa kila mwananchi na wadau mbalimbali katika kukabiliana tatizo la rushwa nchini.