Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) Bw.James Sando akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo ya matumizi rasmi ya moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa kieletroniki Jijini Mwanza
Kamishna wa sera ya ununuzi kwa umma Dkt.Frederick Mwakibinga akiwasilisha hotuba kwa niaba ya Waziri wa Fedha Dkt.Mwigulu Nchemba kwenye mafunzo ya matumizi rasmi ya moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko kieletroniki kwa mikoa ya Kanda ya ziwa
……………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imeokoa Bilioni 583 baada ya kuzuia utoaji tuzo kwa zabuni 35 kwa wazabuni wasio na uwezo wa kifedha pamoja na wale waliokosa sifa za kitaalamu za kutekeleza zabuni za miradi mbalimbali nchini.
Fedha hizo zimeokolewa ndani ya miaka minne ikiwa ni baada ya Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPRA) kushughulikia mashauri 162 yaliyotokana na michakato mbalimbali ya ununuzi wa umma.
Hatua hiyo iliepusha Serikali kuingia katika mikataba ambayo ingekuwa na utekelezaji wa miradi isiyoridhisha hatua ambayo ingesababisha upotevu wa fedha za umma na kuchelewesha maendeleo stahiki kwa wananchi.
Hayo yamebainishwa Leo Jumanne Feburuari 04, 2025 kwenye mafunzo ya siku tatu ya moduli mpya ya kupokea na kushughulikia malalamiko kupitia mfumo wa Ununuzi wa Kieletroniki (NeST) Jijini Mwanza.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania ambapo yamewakutanisha wazabuni na taasisi nunuzi kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Mwanza,Geita,Simiyu,Mara, Shinyanga na Kagera
Akizungumza katika mkutano huo Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma, James Sando amesema katika kipindi hiki cha uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu PPAA kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha,Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na taasisi zinazosimamia ununuzi wa umma nchini imeweza kushiriki katika kutungwa upya kwa Sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2023 na kanuni za ununuzi wa umma za mwaka 2024.
“Sheria hii mpya ya ununuzi wa umma ilioanza kutumika Juni 2024 na kanuni zake imeleta maboresho mbalimbali katika eneo hili la ununuzi na ugavi ikiwemo kupunguza muda wa kushughulikia malalamiko na rufaa zinazotokana na michakato ya ununuzi wa umma”, Amesema Sando
Aidha, ameeleza kuwa muda wa kuwasilisha malalamiko kwa taasisi nunuzi umepunguzwa kutika siku saba hadi tano za kazi na endapo Afisa Masuhuli ataunda jopo la mapito ya malalamiko atatakiwa kutoa uamuzi wake ndani ya siku saba za kazi.
“Pia muda wa kuwasilisha rufaa PPAA umepunguzwa kutoka siku saba za kazi hadi siku tano za kazi huku muda wa Mamlaka ya Rufani kushughulikia malalamiko au rufaa umepunguzwa kutoka siku 45 hadi 40”,
Awali akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Waziri wa Fedha Dkt.Mwigulu Nchemba Kamishna wa Idara ya Sera ya Ununuzi wa Umma, Dkt. Frederick Mwakibinga amezielekeza taasisi nunuzi zote nchini kuhakikisha zinatumia mfumo wa kieletroniki wa ununuzi wa umma katika kuchakata ununuzi wake kama inavyoelekezwa katika sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2023.
“Taasisi zote ambazo hazitatumia mfumo huo zitaadhibiwa kwa mujibu wa sheria,kanuni na taratibu zilizopo”, Amesema
Aidha, ameiagiza PPAA kwa kushirikiana na PPRA kuhakikisha inatoa elimu na mafunzo ya kutosha kuhusu moduli mpya ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kieletroniki ili kuisaidia Serikali kupata thamani halisi ya fedha zake katika miradi mbalimbali.