Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Mahakama ya Tanzania itakuwa na mchango mkubwa katika kuiwezesha Tanzania kufikia malengo yake ya maendeleo kama yatakayobainishwa kwenye Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo wakati wa maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Sheria nchini na uzinduzi rasmi wa Shughuli za Mahakama kwa mwaka 2025 yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali yakiwa na kaulimbiu “Tanzania ya 2050: Nafasi ya Taasisi zinazosimamia Haki Madai katika kufikia malengo makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo”.
Aidha, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa utekelezaji wa Dira utavutia mitaji ya uwekezaji jambo litakalohitaji kuingia mikataba mbalimbali baina ya Serikali na sekta binafsi. Hivyo, ametoa rai kwa sekta zote zinazohusika na Haki Madai kujiandaa vyema katika kutoa huduma za haki.
Rais Dkt. Samia pia ameeleza kuwa katika miaka ijayo Tanzania inatarajia kuhushuhudia ongezeko kubwa la shughuli za kibiashara na kiuchumi, hali itakayoongeza uhitaji wa huduma za utoaji haki zinazohusiana na biashara hizo.
Kwa msingi huo, Rais Dkt. Samia ameitaka Mahakama ya Tanzania na Mabaraza ya Mashauri ya Kodi kuwa wawezeshaji wa shughuli za kiuchumi kwa kutenda haki kwa usawa na kwa wakati.
Vilevile, Rais Dkt. Samia amempongeza Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma na mhimili wa Mahakama ya Tanzania kwa maendeleo yanayoendelea kushuhudiwa katika utekelezaji wa huduma za sheria, ikiwemo kuimarisha matumizi ya TEHAMA na msisitizo wa kisera unaowekwa na Mahakama katika kuimarisha
Sharifa B. Nyanga
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu