Na Baltazar Mashaka, Mwanza
WAISLAMU mkoani Mwanza, kwa kushirikiana na viongozi wa dini na siasa,wamemuombea dua Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, wakisema kuwa maendeleo makubwa yanayoendelea kutekelezwa chini ya uongozi wake ni ishara ya upendo na umoja wa kitaifa.
Dua hiyo imefanyika nje ya Msikiti wa Sheikh Abubakar Zubeir Bin Ally, leo na kuhusisha viongozi wa dini,waumini wa dini ya Kiislamu, wananchi wakiwemo viongozi na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (JUWAKITA), Amina Masenza,ameeleza kuwa Rais Samia amekuwa mkombozi kwa Watanzania, hasa wanawake, kutokana na miradi ya maendeleo aliyotekeleza ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya maji, umeme na huduma bora za afya.
Amesema, “Akinamama wamepata nafuu kutokana na miradi ya maji,ametutua ndoo kichwani,ameboresha huduma za afya na sasa tunapata huduma kwa urahisi zaidi,huku pia tukiendelea kumshukuru kwa uteuzi wa wanawake katika nafasi za uongozi.”
Masenza ameongeza kuwa, hatua ya Rais Samia kutoa kipaumbele kwa wanawake katika maendeleo ni kielelezo cha uongozi wa kipekee na ni muhimu kwa Watanzania kuendelea kumuombea dua ili aendelee kufanya kazi nzuri kwa ajili ya taifa.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana,Peter Begga, amesisitiza kuwa Rais Samia anastahili kuombewa kutokana na juhudi zake za kuleta maendeleo.
“Miradi ya kimkakati kama Daraja la Kigongo-Busisi limekamilika na SGR inakwe kwa kasi,jambo ambalo lilinaonekana kama ndoto.Rais Dk. Samia amedhihirisha uongozi bora na amani,” amesema Begga.
Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke,amesisitiza kuwa kumuombea Rais Samia ni wajibu wa kila Mtanzania, na kwamba dua ni nguvu kubwa inayoweza kuimarisha amani na umoja wa taifa.
“Tanzania tuna Rais mmoja, na ni lazima tumwombee dua ili aendelee kutuletea maendeleo.Uchawa (kujipendekeza) si jambo baya, na hata katika Uislamu, tunajifunza kuwa mtiifu kwa viongozi wetu na ili uwe muumini mzuri lazima uwe chawa wa Mtume Muhhamad S.A.W,” amesema Sheikh Kabeke.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amewapongeza Waislamu mkoani humu kwa kuonesha mshikamano na upendo kwa Rais Samia.
Amesisitiza kuwa dua ni chakula cha nafsi na roho,inasaidia viongozi kuwa na nguvu ya kupambana na changamoto mbalimbali wakiwemo maadui wasiowafahamu .