Na Mwandishi wetu, Mirerani
WAFANYABISHARA wa madini ya Tanzanite wa mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamempongeza Mkurugenzi wa kampuni ya Chusa Mining LTD, Joseph Mwakipesile kwa kufanikisha mnada wa madini kwenye eneo hilo.
Katika mnada huo uliofanyika ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite gramu 4,874.16 za madini ya Tanzanite zenye thamani ya shilingi milioni 21,430,000 ziliuzwa na kufanikisha mapato ya Serikali shilingi milioni 1,500,100.
Wakizungumza baada ya kufanyika kwa mnada huo baadhi ya wafanyabishara hao wamempongeza Mkurugenzi wa kampuni ya Chusa Mining LTD, Joseph Mwakipesile kwa kutoa madini yake kwenye mnada huo.
Mmoja kati ya wafanyabishara hao Sila Akede amesema kitendo cha Chusa Mining LTD, kutoa madini yake ili yauzwe kwa kufanyiwa mnada kwa wafanyabishara hao kinapaswa kupongezwa.
Sila amesema ni wakati sasa kwa wachimbaji madini wengine ambao migodi yao inazalisha kuwaunga mkono wafanyabishara wa Tanzanite kwa kufanya minada kila wakati.
Mfanyabiashara mwingine, Ambrose Ndege amempongeza mchimbaji wa madini Joseph Mwakipesile kupitia kampuni ya Chusa Mining Ltd, kwa kufanikisha mnada huo.
“Chusa amefanya jambo kubwa la kuweka madini yake kwenye mnada tofauti na angekuwa anauza kwa mtu mmoja mmoja ila hii imekuwa na tija kwa wafanyabishara wote,” amesema Ndege.
Mfanyabiashara mwingine, Lidya Mollel amesema minada kama hiyo iliyofanywa na Chusa inapaswa kufanyika kila mara ili kuchochea uchumi wa eneo hilo la mji mdogo wa Mirerani.
“Tunapaswa kuwashukuru wachimbaji hawa akiwemo Chusa kwa kufanya minada hii kwani inasaidia kuwanyanyua kiuchumi katika mji mdogo wa Mirerani,” amesema Mollel.