Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, ametoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi waliopata mikopo ya serikali kuhakikisha wanazitumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuzirejesha kwa wakati ili kuwezesha wengine kupata fursa hiyo.
Akizungumza leo Januari 31, 2025, jijini Dar es Salaam na wadau wa sekta ya benki, huduma za kifedha kwa njia ya simu na wadau wa huduma za kifedha kidijitali, Gavana Tutuba amesema Benki Kuu inaendelea kuboresha mifumo ya urejeshaji wa mikopo ili kurahisisha mchakato huo kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Tutuba, mfumo wa marejesho ni muhimu katika kujenga uaminifu na kuhakikisha mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi unajitosheleza kwa muda mrefu. “Serikali imeweka mifumo bora ya urejeshaji ili wananchi wanufaike kwa kupata mikopo kwa gharama nafuu na kurahisisha shughuli zao za kiuchumi,” amesema.
Katika juhudi za kuhakikisha urejeshaji wa mikopo unakuwa rahisi, Kampuni ya Airpay Tanzania imeanzisha mfumo wa Loan Management System unaounganisha benki na mitandao ya simu ili wananchi waweze kulipa marejesho yao kirahisi kupitia mawakala wa malipo. Makamu wa Rais na Meneja Mikakati wa Airpay Tanzania, Mihayo Wilmore, amesema mfumo huu utasaidia kupunguza ucheleweshaji wa marejesho na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa madeni.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Juma Barhan Mohamed, amesema mfumo huu utawasaidia wananchi wa Zanzibar kulipa mikopo bila kikwazo cha kusafiri, hivyo kupunguza changamoto zilizokuwa zikisababisha mikopo chechefu.
Mohamed amepongeza benki na kampuni za simu, hususan Airtel na Benki ya TCB, kwa kuwa miongoni mwa taasisi za kwanza kushirikiana na Airpay katika kuanzisha mfumo huu wa kidijitali. “Hatua hii ni muhimu katika kufanikisha azma ya kufikia uchumi wa kidijitali ifikapo mwaka 2030,” amesema.
Serikali na wadau wa kifedha wanatarajia kuwa mfumo huu wa malipo kidijitali utaleta mageuzi makubwa katika urejeshaji wa mikopo, kupunguza kiwango cha mikopo chechefu, na kusaidia wananchi kujenga biashara endelevu kupitia mikopo nafuu ya serikali.