Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza Idirisa Kisaka akitoa taatifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya zaidi ya billion nne
………………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza imefanikiwa kudhibiti kiasi cha zaidi ya Shilingi Milioni 300 katika eneo la ukusanyaji wa kodi ya zuio TRA pamoja na eneo la mnada wa mifugo Wilaya ya Misungwi.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi 13 ya maendeleo kwa waandishi wa habari katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2024, Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Idrisa Kisaka ameeleza kuwa wamekuwa wakifuatilia na kubaini ubadhilifu huo wa fedha.
Kisaka ameeleza kuwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo 13 kwenye sekta ya Elimu, Barabara na Biashara yenye thamani ya zaidi ya sh Bil 4.4 miradi 12 yenye thamani ya shilingi 3,910,877,146 imekutwa na mapungufu.
“Ufuatiliaji huo wa TAKUKURU umesaidia utekelezaji wa mapendekezo kwa zaidi ya asilimia 65.2 na kupelekea miradi hiyo kuwa na ubora kwa kiwango kilichokusudiwa” Amesema Kisaka.
Amesema kwenye eneo la Elimu kwa umma TAKUKURU mkoani humo katika kilele cha mbio za mwenge wa uhuru 2024 imefanikiwa kutoa elimu na kubandika mabango yenye ujumbe wa kukemea vitendo vya rushwa katika maeneo ya wazi na yenye mkusanyiko mkubwa wa watu wengi.
Akizungumzia mikakati ya robo ya tatu ya mwaka 2024/2025 Kisaka amesema TAKUKURU Mkoa wa Mwanza imepanga kufuatilia taatifa za vitendo vya rushwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kabla,wakati na baada ya uchaguzi na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria.
Aidha, amesema imepanga kuendelea kusimamia mashauri yote yaliyoko Mahakamani ikiwa ni pamoja na kufungua mashauri mapya.
Mwisho alitoa ushauri kwa wananchi kushirikiana na TAKUKURU kuzuia vitendo vya rushwa kwenye maeneo yote ya utoaji wa huduma,kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo na katika zoezi zima la uchaguzi.