Bunge la Tanzania limepitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Kazi (NA.13) wa Mwaka 2024 ambao umeongeza likizo ya uzazi kwa wanaojifungua Watoto njiti ambapo likizo kwa anayejifungua Watoto njiti itaanza kuhesabiwa wiki 40 baaada ya Mama kujifungua huku Baba wa Mtoto njiti akipewa likizo ya siku saba kutoka likizo ya siku tatu.
Waziri Anthony Mavunde ameyasema hayo leo January 31,2025 Bungeni Jijini Dodoma alipokuwa akiwasilisha maelezo ya muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Kazi wa Mwaka 2024 (The Labour Laws (Amendments) Bill, 2024) zinazolenga kuleta ustawi katika sekta ya kazi nchini, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete.
Huu ni utekelezaji wa maombi yaliyotolewa na Chama cha Wafanyakazi katika Sherehe za Wafanyakazi (Mei Mosi) zilizofanyika May 01 Mei 2024 Mkoani Arusha ambapo Mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango kwa niaba ya Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Wadau mbalimbali ambao ni Waanzilishi wa wazo hilo wakiwemo Taasisi ya Doris Mollel ambayo inajihusisha na kusaidia watoto wanalizaliwa kabla ya wakati nchini, pamoja na Mtandao wa Haki ya Afya ya Uzazi nchini wamepongeza suala hilo ambalo wamekuwa wakilipigania kwa muda mrefu.