Mhe. Phaustine Kasike, Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji amekutana na Mkurugenzi Mkuu wa ATCL Mhandisi Peter Ulanga.
Mkutano huo ulifanyika kwenye Ofisi za ATCL zilizopo eneo la Uwanja wa Ndege wa Zamani Dar es Salaam (Terminal One), tarehe 30 Januari, 2025.
Katika mazungumzo yao, Mhandisi Ulanga ameeleza nia ya Shirika la ATCL kuanza safari za kwenda nchini Msumbiji ili kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii baina ya nchi hizo mbili zenye uhusiano wa kidugu na kihistoria.
Aidha, Mhandisi Ulanga ameongeza kuwa ATCL inadhamiria kuanzisha mchakato hivi karibuni wa kushughulikia taratibu za kitaalamu zinazohitajika kuwezesha safari hizo kuanza.
Kwa upande wake, Mhe. Balozi Kasike aliahidi kutoa kila aina ya ushirikiano kwa ATCL ili kufanikisha azma hiyo.