Na Sophia Kingimali.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Albert Chalamila amesema kuwa uongozi wa mkoa wa mkoa huo unatarajia kufanya mazungumzo na Shirika la Reli nchini (TRC) ili kuangalia kama kutakuwa na uwezekano wa kujenga reli yakusafirisha abiria ndani ya mkoa ili kupunguza msongamano na kurahisisha ufanyaji wa biashara kwa saa 24.
Akizungumza leo Januari 30,2025 wakati akitoa mrejesho wa mkutano wa nishati Afrika uliofanyika siku mbili,Mkuu wa mkoa amesema lengo la treni hiyo ni kupunguza adha ya usafiri kwa mkoa wa Dar es Salaam ambapo reli hiyo itajengwa kwa fedha za ndani ambazo zinakusanywa kwenye halmashauri.
“Fedha tunazozikusanya kwa mkoa wa Dar es Salaam zinafika si chini ya Sh bilioni 300 Jumanne ijayo tutakaa pamoja na Mkurugenzi wa TRC kuangalia namna yakujenga reli ya kawaida inayobeba abiria ambayo itakuwa ni ubia TRC na watu binafsi na halmashauri,”amesema Chalamila.
Amesema ujenzi wa reli hiyo na njia ambayo itajengwa utajulikana baada ya watalaam kufanya upembuzi yakinifu na kuona sehemu gani inapaswa kujengwa.
Mbali na hilo Chalamila pia ametangazwa kuanza kwa utaratibu wa wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa masaa 24 kuanzia Februari 22 mwaka huu.
“Katika kuelekea kufungua zaidi mkoa wa Dar es Salaam mimi na wenzangu tumekubaliana Dar es Salaam ianze kufanya biashara saa 24,kwa maana hiyo Februari 22 ndio itakuwa siku rasmi yakufungua.
“Awali tulipanga Februari 8,2025 lakini tumepeleka mpaka Februari 22 kwa sababu kuna baadhi ya maeneo hatujafika kuyaweka taa na maboresho mengine madogo madogo,”amesema Chalamila.
Mbali na hilo ofisi ya mkuu ya mkoa wamekubaliana mambo mbalimbali kutokana na mji huo kukua kwa kasi ikiwemo masuala kuboresha majengo chakavu.
“Kutokana na mji wetu kukua kwa kasi tumekubaliana yafuatayo kuunda kamati maalum kuangalia majengo chakavu na yaliyochoka,baada ya hapo kamati itashirikiana na wenye majengo kutafuta wafadhili ili kuyaboresha majengo hayo yaendane na taswira ya Jiji la Dar es salaam”amesema Chalamila.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya wafanyabiashara Kariakoo Hawa Ghasia amemshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kutoa pesa kwa ajili ya kuboresha soko dogo la kariakoo ambalo limegharimu kiasi cha bilioni 28.03 ambapo mpka sasa marekebisho hayo yamefikia asilimia 97 na wanatarajia kuanzia kesho Januri 31,kupandisha majina ya wafanyabiashara waliokuwepo awali kabla ya soko hilo halijaungua.
“Kesho tunaanza zoezi la kupandisha majina ya wafanyabiashara wa awali,nitoe rai ambao wanadaiwa walipe madeni yao ili kupunguza usumbufu wakati wa kugawa vizimba lakini wale ambao ni wafanyabiashara wapya wanapaswa kutulia na wasidanganyike kama kuna mtu kati watamlipa ili wapate nafasi bali nafasi hizo zitaombwa kwa kutumia mfumo wa TAUSI na hivi karibuni tutakutana nao na tutawaelekeza jinsi ya kutumia mfumo huo kuomba nafasi”,Amesema Ghasia.