Farida Mangube, Morogoro
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Raphael Chibunda, amewataka wanafunzi waliopata ufadhili wa masomo kutoka taasisi ya CAN TANZANIA kutumia fursa hiyo kwa bidii, kuwa na nidhamu, na kuhakikisha wanafikia malengo yao ya kielimu.
Prof. Chibunda alitoa wito huo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wanaosaidiwa na CAN TANZANIA. Amesisitiza kuwa SUA ni miongoni mwa taasisi za elimu zilizonufaika na mpango huo, huku akihimiza taasisi hiyo kupanua wigo wa ufadhili ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi wanaokabiliwa na changamoto za kifedha.
Mwenyekiti wa Bodi ya CAN Tanzania, Dkt. Catherine Aloyce Masau, amesema kuwa shirika hilo limefadhili wanafunzi 36 kutoka vyuo mbalimbali nchini, vikiwemo vya Tanzania Bara na Zanzibar. Ufadhili huo unahusisha wanafunzi wa ngazi tofauti za elimu, ikiwemo shahada za uzamili, diploma, na vyeti. Amebainisha kuwa mpango huo unawalenga wanafunzi wa jinsia zote, hasa wale kutoka familia zenye hali duni.
“Watanzania wengi wanakabiliwa na changamoto za kugharamia masomo yao na mara nyingi hutegemea ufadhili wa serikali. Kama CAN Tanzania, tumeona ni muhimu kusaidia juhudi hizo kupitia mpango huu wa ufadhili,” alisema Dkt. Masau.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa CAN Tanzania, Dkt. Sixbert Mwanga, alieleza kuwa vigezo muhimu vya kupata ufadhili ni hali ya kifamilia ya mwanafunzi na kozi anayosomea, ambayo inapaswa kuwa na mchango wa moja kwa moja katika jamii. Aliongeza kuwa wanafunzi wanaofadhiliwa wanapaswa kudumisha viwango bora vya ufaulu ili kuendelea kunufaika na mpango huo.
Mmoja wa wanufaika wa ufadhili huo, Ampelius Anthony, mwanafunzi wa Tiba ya Mifugo SUA, alieleza kuwa safari yake ya elimu ilikuwa na changamoto kubwa, lakini kupitia ufadhili huo, sasa anaweza kuendelea na masomo yake bila vikwazo vya kifedha.
“Ufadhili huu umekuja wakati sahihi na utanisaidia kutimiza malengo yangu ya kielimu,” alisema Ampelius.
Aidha, alitoa wito kwa mashirika mengine kuiga mfano wa CAN Tanzania kwa kusaidia wanafunzi wenye uhitaji ili kuwasaidia kufanikisha ndoto zao.
Mpango huu wa ufadhili kutoka CAN Tanzania umeleta faraja kwa wanafunzi wengi nchini, huku ukihamasisha bidii katika masomo na kuwasaidia vijana wa Kitanzania kujenga mustakabali mzuri wa maisha yao.