Na Sophia Kingimali.
KAIMU Mkuu wa Chuo Cha Ufundi Cha Furahika – Veta, Dkt David Msuya, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa ujio wa marais 25 katika Mkutano wa Nishati ‘Afrika Energy Summit’ambao umeanza, Januari 27, 2025 jijini Dar es Salaam kwani mkutano huo utaenda kufungua fursa nyingi za uwekezaji katika sekta ya nishati Afrika.
Lengo la mkutano huo ambao umewaleta pamoja viongozi hao na wadau katika sekta ya Nishati kujadili mikakati ya kukabiliana na changamoto za nishati na kuchangamkia fursa zilizopo Afrika.
Pia moja ya matokeo makubwa ni kupitishwa kwa Azimio la Dar es Salaam linaosisitiza dhamira ya viongozi wa Afrika kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu na endelevu kwa maendeleo ya Bara la Afrika ambapo Mkutano huo unafikia tamati leo, Januri 28, 2025.
Dk Msuya akizunguza na Waandishi wa Habari leo Januari 8,2025, jijini Dar es Salaam, amesema mkusanyiko wa viongozi hao hapa nchini wa kujadilia masuala ya nishati ni jambo jema kwa maana inakuwa sehemu ya kuchochea uchumi wa nchi na Afrika kwa ujumla.
“Nampongeza Rais wetu mpendwa kwa jambo hili kubwa Afrika na hii inatoa fursa kwa uchumi wetu kuongezeka naamini pia katika kipindi hiki cha siku mbili za mkutano huu, Watanzania wameutumia vema kwa kujiongezea kipato hususan katika hoteli na maeneo mengine ya huduma,” amesema.
Mkutano huo umekutanisha wakuu wa nchi za Afrika takribani 54 wakiwemo Mawaziri wa Fedha na Nishati, Marais wa Benki ya Dunia na Maendeleo ya Afrika, viongozi wa Jumuia ya Ulaya na Jumuia ya Afrika.
Akizungumzia kuhusu maendeleo ya Chuo chake Dkt Msuya ameweka wazi kuwa bado wanaendelea kusahili wanafunzi wapya wa kozi fupi na ndefu, hivyo ameomba wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kusoma kozi mbalimbali ikiwemo Hoteli, umeme, ukatishaji tiketi za ndege,utoaji huduma kwenye ndege, udereva na nyinginezo.
“Tunakaribisha wanafunzi wote waliotoka shuleni waache kukaa mtaani waje kusoma hapa kwani elimu ni bure, Serikali imewezesha watoto wote ambao wamekosa fursa ya kuendelea na elimu kwa sababu mbalimbali, hivyo waache kukaa nyumbani waje kusoma kozi zitakayowasaidia kuendesha maisha yao na tunahitaji wanafunzi zaidi ya 200, pia baada ya kuhitimu tunawasaidia kupata ajira kwenye masoko mbalimbali ya ajira nchini” amesisitiza.
“Pia hata walimu wanaofundisha masomo ya Amali katika maeneo mbalimbali nchini waje kwetu kujifunza kwa muda mfupi ili huko walipo watoe elimu bora kwa maslahi mapana kwa jamii na nchi kwa ujumla na wazazi wote watumia fursa za mtoto kusoma bure,” amesema.