Rais wa Jamhuri ya Malawi, Mheshimiwa Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera, amewasili jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati.
Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati unafanyika tarehe 27 na 28 Januari 2025 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere.
Alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mheshimiwa Dkt. Chakwera alilakiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Mhe. Dkt. Saada Mkuya, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi na maafisa waandamizi wa serikali
Mkutano huo unawaleta pamoja Wakuu wa Nchi za Afrika, wataalam wa nishati, viongozi wa sekta binafsi, na washirika wa maendeleo kwa ajili ya kujadili mikakati ya kukabiliana na changamoto za nishati na kuchangamkia fursa za bara la Afrika. Moja ya matokeo muhimu ya mkutano huo ni kupitishwa kwa Azimio la Dar es Salaam, linalosisitiza dhamira ya pamoja ya viongozi wa Afrika kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu, na endelevu kwa maendeleo ya bara hili.