Tanzania imeandika historia kwa kuwa mwenyeji wa Mkutano Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati, utakaofanyika Januari 27 na 28, 2025, jijini Dar es Salaam, huku idadi ya viongozi wa ngazi ya juu watakaoshiriki ikiwa ni kubwa zaidi katika historia ya nchi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, mkutano huo utahudhuriwa na Wakuu wa Nchi 25, Makamu wa Rais wawili, Mawaziri Wakuu wanne, na Naibu Mawaziri Wakuu wawili, na kufanikisha idadi ya viongozi wa ngazi za juu 35.
“Tanzania haijawahi kupokea idadi kubwa ya viongozi wa ngazi ya juu kama hawa katika tukio moja. Tukiangalia matukio ya awali, tulipokea Wakuu wa Nchi 19 wakati wa kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere mwaka 1999, na Wakuu wa Nchi 15 wakati wa Mkutano wa SADC mwaka 2019. Mkutano huu unazidi kwa ukubwa,” alisema Balozi Kombo.
Nchi zilizothibitisha kushiriki ni pamoja na Algeria, Kenya, Nigeria, Ghana, Ethiopia, Zambia, Sudan, Somalia, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na nyinginezo. Makamu wa Rais kutoka Gambia na Benin pamoja na Mawaziri Wakuu kutoka Cote d’Ivoire, Uganda, São Tomé and Príncipe na Equatorial Guinea watashiriki pia.
Balozi Kombo alibainisha kuwa mkutano huu ni matokeo ya juhudi za diplomasia ya kimataifa zinazotekelezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Mwaliko wa Rais Samia katika Mkutano wa Nchi 20 Tajiri zaidi duniani (G20) nchini Brazil Novemba 2024, na nafasi aliyopewa kuzungumza kwa niaba ya Afrika kwenye Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya Afrika na China (FOCAC), ni ishara ya kuimarika kwa nafasi ya Tanzania duniani,” alisema.
Balozi Kombo pia alisisitiza kuwa mikutano ya kimataifa kama huu ina faida kubwa kwa uchumi wa ndani, hususan sekta ya utalii, hoteli, usafiri, na wajasiriamali wadogo kama mama lishe na boda boda, akisema kuwa inatoa fursa ya kipekee ya kukuza mapato ya wananchi wa kawaida.
Akihitimisha, Waziri Kombo aliwapongeza waandishi wa habari kwa mchango wao mkubwa wa kuelimisha umma na kuwaomba kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha habari za mkutano huu zinawafikia Watanzania na jumuiya ya kimataifa.
“Mkutano huu ni tukio la kihistoria, na tunawategemea nyinyi waandishi wa habari kuifanya Tanzania izidi kung’ara,” alihitimisha.