Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akikata utepe katika hafla ya uzinduzi mashirikiano baina ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Kampuni ya Azam Marine kwa ajili ya kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria kwa njia ya majini kutoka Kigamboni kwenda Magogoni iliyofanyika leo Januari 23, 2025, Magogoni, Dar es Salaam (PICHA NA NOEL RUKANUGA)
Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega akikagua mfumo wa kisasa wa kukusanya mapato utakaotumika katika kivuko cha Magogoni,Dar es Salaam baada ya Kampuni ya Azam Marine kufanya uwekezaji.
Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega, Mtendaji Mkuu wa TEMESA Bw. Lazaro Kilahala, Mkurugenzi Mtendaji wa Azam Marine Abubakar Aziz Salim, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Albert Chalamila, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam Abbas Mtevu pamoja na viongozi wengine wakiwa katika picha ya pamoja wakati wakikagua miundombinu ya Kivuko cha Magogoni baada ya Kampuni ya Azam Marine kufanya maboresho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Azam Marine Abubakar Aziz Salim (kushoto) akitoa ufafanuzi wa jambo kwa Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega wakiwa ndani ya kivuko kipya cha kipya cha Azam Marine wakati wakivuka kutoka Magogoni kwenda Kivukoni Kigamboni
Muonekano wa vivuko viwili vya mwendokasi vya Kampuni ya Azam Marine kwa ajili ya kutoa huduma ya kuvusha wananchi kutoka Magogoni kwenda kivukoni Kigamboni.
Mkurugenzi Mtendaji wa Azam Marine Abubakar Aziz Salim akizungumza jambo katika hafla ya uzinduzi wa mashirikiano baina ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kwa ajili ya kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria kwa njia ya majini kutoka Kivukoni Kigamboni kwenda Magogoni iliyofanyika leo Januari 23, 2025, Magogoni, Dar es Salaam.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Mhe. Mussa Azzan Zungu akizungumza jambo katika hafla ya uzinduzi wa mashirikiano baina ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Kampuni ya Azam Marine kwa ajili ya kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria kwa njia ya majini kutoka Kivukoni Kigamboni kwenda Magogoni iliyofanyika leo Januari 23, 2025, Magogoni, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam Abbas Mtevu akitoa salamu za Chama katika hafla ya uzinduzi wa mashirikiano baina ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Kampuni ya Azam Marine kwa ajili ya kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria kwa njia ya majini kutoka Kivukoni Kigamboni kwenda Magogoni iliyofanyika leo Januari 23, 2025, Magogoni, Dar es Salaam.
Picha za matukio mbalimbali hafla ya uzinduzi wa mashirikiano baina ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Kampuni ya Azam Marine
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega amezindua Mashirikiano baina ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Kampuni ya Azam Marine kwa ajili ya utoaji wa huduma ya usafirishaji wa abiria kwa njia ya majini kutoka Kivukoni Kigamboni kwenda Magogoni jambo ambalo litasaidia kumaliza changamoto ya wananchi kukaa muda mrefu kusubiri kivuko.
Katika mashirikiano hayo pamoja na mambo mengine kampuni ya Azam Marine imefanya uwekezaji wa shilling bilioni 5.98 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kupumzikia abiria, Ofisi pamoja na kuweka mfumo rafiki ya kukusanya mapato.
Akizungumza leo Januari 23, 2025 jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa mashirikiano baina ya TEMESA na Kampuni ya Azam Marine, Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega, amesema kuwa uwekezaji uliofanya na Azam Marine wa kutoa huduma ya usafirishaji kutoka kigamboni hadi magogoni utasaidia kupunguza msongamano wa watu na kumaliza changamoto ya upotezaji wa muda.
Mhe. Ulega amesema kuwa vivuko hivyo vimekaguliwa na salama kwa viwango vya kimataifa kwa ajili ya kufanya shughuli ya usafirishaji abiria na kuondoa changamoto ya wananchi kusubiri kuvuko kutoka zaidi ya dakika 45 hadi dakika tano.
“Nawapongeza Kampuni ya Azam Marine kwa kufanya uwekezaji huu ambao unakwenda kuwasaidia wananchi wa Kigamboni, muendelee kupeana ushirikiano nyinyi wote ili kuhakikisha watanzania wanakuwa salama wakati wote wa matumizi wa vyombo hivi” amesema Mhe. Ulega.
Mhe. Ulega amesema vivuko vya serikali vitaendelea kutoa huduma kufanya kazi kama kawaida, huku akitoa wito kwa Azam Marine kwenda kuwekeza katika maeneo mengine ya nchi ili kurahisha usafiri wa majini kwa wananchi.
Mtendaji Mkuu wa TEMESA Bw. Lazaro Kilahala, amesema kuwa kituo cha magogoni, Dar es Salaam kimekuwa kikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa vivuko pamoja na hitilafu za mara kwa mara na kusababisha malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.
Bw. Kilahala amesema kwa kawaida kivuko hiko kina hudumiwa na vivuko vitatu Mv Magogoni, Mv Kigamboni na Mv Kazi lakini kwa sasa kuna kivuko kimoja ambacho kinatoa huduma baada ya vingine kuwa katika matengenezo.
Amesema kuwa baada ya mashirikiano hayo Azam Marine wataongeza vivuko na kutoa huduma ya kusafirisha abiria kwa njia ya majini na kutoa fursa kwa wananchi kuchangua kivuko.
Bw. Kilahala Azam watatoza nauli ya shilingi mia tano, huku akifafanua kuwa mashirikiano hayo yatadumu kwa muda wa miaka nane na kila baada ya miaka mitatu watakuwa wanapitia makubaliano.
Mkurugenzi Mtendaji wa Azam Marine Abubakar Aziz Salim, amesema kuwa kupitia uwekezaji wameweza kutoa ajira ya moja kwa moja 470 nchini na kufanikiwa kuhudumia abiria milioni mbili kwa mwaka Tanzania Bara na Zanzibar.
Amesema kuwa vikuko hivyo viwili vitakuwa vinaanza kutoa huduma kila siku kuanzia saa 11:00 alfajiri hadi saa 5:00 usiku, huku akieleza kuwa kwa saa vitahudumia abiria 5,000 “Vivuko vinne vinaendelea kujengwa na kabla ya mwezi Mei, 2025 vitaanza kutoa huduma”
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Albert Chalamila amesisitiza umuhimu wa kuwapa sekta binafsi kufanya uwekezaji wa kutoa huduma kwa ufanisi zaidi, huku akitoa wito kwa kampuni ya Azam Marine kuongeza wigo wa kufanya uwekezaji katika maeneo mbalimbali ya Nchi.