DAR ES SALAAM
Rais wa mpito wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré, ni miongoni mwa marais 25 watakaoshiriki mkutano mkubwa wa nishati utakaofanyika jijini Dar es Salaam, Januari 27-28, 2025.
Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia masuala ya nishati na mabadiliko ya hali ya hewa, Dk. Kevin Kariuki, amesema mkutano huo pia utawakutanisha mawaziri wa fedha na nishati 60 wa Afrika pamoja na viongozi wa kimataifa.
Katika mkutano huo, wakuu wa nchi wa Afrika wanatarajiwa kusaini Mpango Mahususi wa Nishati wa Afrika (Africa Energy Compact), ambao awamu yake ya kwanza itahusisha nchi 14 zikiwemo Tanzania, Burkina Faso, Malawi, Chad, Nigeria, DRC, Niger, Liberia, Msumbiji, Madagascar, Zambia, Mali, Ivory Coast, na Mauritania.
Kapteni. Ibrahim Traoré, aliyepata uongozi wa mpito mnamo Oktoba 2022 kupitia mapinduzi ya kijeshi, amejitokeza kuwa mmoja wa viongozi wa Kiafrika wanaochukua hatua thabiti za kulinda maslahi ya nchi zao. Akiwa na umri mdogo kwa rais, miaka 35, Traoré ameonyesha msimamo wa kupigania uhuru wa kiuchumi, kutetea rasilimali za taifa lake, na kuhakikisha kwamba maendeleo ya Burkina Faso yanazingatia mahitaji ya wananchi wa kawaida.
Traoré anaamini katika kujenga mifumo ya kitaifa inayowezesha watu wa chini, hususan katika sekta za kilimo, elimu, na nishati. Ameshikilia kwamba Burkina Faso haitaendelea kutegemea msaada wa nje pekee bali itatumia rasilimali zake za ndani kwa maendeleo endelevu.
Katika mkutano wa Dar es Salaam, ushiriki wa Traoré unatarajiwa kuelekeza mjadala katika umuhimu wa nishati kama nguzo ya maendeleo barani Afrika. Burkina Faso, ambayo imekuwa ikikumbwa na changamoto za kiusalama na kiuchumi, inajitahidi kuongeza upatikanaji wa umeme hususan vijijini, ambapo kiwango cha umeme bado ni chini ya asilimia 25.
Traoré pia amekuwa akihimiza ushirikiano wa kanda katika miradi ya nishati kama njia ya kupunguza utegemezi wa mafuta na kuwekeza katika vyanzo vya nishati mbadala kama jua na upepo.
Mkutano huo unaodhaminiwa na Benki ya Dunia, AfDB, na washirika wengine wa maendeleo, unalenga kuhakikisha watu milioni 300 barani Afrika wanapata huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030. Ushirikiano kati ya nchi 14 za awamu ya kwanza ya mpango huo unatarajiwa kuongeza uwekezaji wa nishati na kupunguza ukosefu wa umeme unaokwamisha maendeleo katika sekta mbalimbali za uchumi.
Kwa msimamo wake thabiti wa kulinda rasilimali na kushirikisha wananchi katika maamuzi, Rais Traoré anabaki kuwa sauti muhimu katika mijadala ya maendeleo barani Afrika.
Ushiriki wake katika mkutano wa Dar es Salaam unatarajiwa kuleta mchango muhimu kwa maono ya Afrika yenye nguvu ya nishati na uchumi endelevu.