Shirika la Posta Tanzania limeanzisha huduma mpya iitwayo Swifpack, inayolenga kuchukua vifurushi na abiria kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa urahisi kupitia simu janja.
Huduma hiyo itazinduliwa rasmi Januari 24, 2025, katika makao makuu ya Shirika la Posta Tanzania jijini Dar es Salaam. Meneja wa Shirika la Posta Tanzania mkoani Mara, Joyce Chirangi, alieleza kuwa huduma hiyo inalenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kurahisisha usafirishaji wa mizigo na abiria.
“Huduma ya Swifpack inalenga kuboresha utoaji wa huduma zetu kwa wananchi. Sio tu huduma za posta bali pia mahitaji ya kila siku ya wananchi kama usafirishaji wa mizigo na abiria,” alisema Joyce.
Chirangi aliongeza kuwa huduma hii itakuwa ya kwanza ya aina yake mkoani Mara, ikisaidia kurahisisha usafiri hasa kutokana na ukubwa wa jiografia ya mkoa huo.
“Kwa mfano, mtu aliyeko Tarime anaweza kununua mzigo na kuomba usafirishwe moja kwa moja hadi alipo. Huduma hii itasaidia sana kuokoa muda na kuongeza ufanisi kwa wateja,” aliongeza.
Huduma ya Swifpack imepangwa kuwa mkombozi wa muda na mahitaji ya usafiri kwa wananchi, huku ikihakikisha mizigo inafika salama na kwa wakati.