Na Farida Mangube
Jumuiya ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUASO) imepongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuandaa Sera mpya ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi pamoja na kuboresha mitaala inayolenga mahitaji ya sasa, kumkomboa mwananchi wa kawaida, na kukabiliana na changamoto za soko la ajira duniani.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi SUA, Bw. Hatibu Kilenga, akizungumza na waandishi wa habari, alisema kuwa sera hiyo mpya imejikita katika kutatua changamoto zinazokabili sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo ambacho kina upungufu wa wataalamu kwa karibu asilimia 66. Pia, ameeleza kuwa sera hiyo inalenga kuwajengea wanafunzi maarifa ya kuleta mabadiliko siyo tu kwa ajili ya kuajiriwa bali pia kujiajiri.
“Kwa mfano, katika eneo la sayansi na teknolojia, sera imeweka mazingira ya upatikanaji wa kitabu bora cha kujifunza, tofauti na zamani ambapo kulikuwa na vitabu vingi vilivyomchanganya mwanafunzi badala ya kumsaidia kuelewa,” alisema Kilenga.
Felister Mwakapeja, Waziri wa Jinsia na Watu wenye Mahitaji Maalumu katika Serikali ya Wanafunzi SUA, alieleza kuwa sera hiyo inaonyesha juhudi za serikali katika kuhakikisha elimu inapatikana kwa wote bila ubaguzi wa rangi, jinsia, au mahitaji maalumu. Pia, amepongeza jitihada za serikali katika kutengeneza mazingira salama ya kujifunza kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu, sambamba na kuboresha mitaala ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira.
Naye Makame Ally, Waziri wa Katiba, Sheria, Bunge na Utawala Bora katika Serikali ya Wanafunzi SUA, alisema kuwa mpango wa elimu huria uliowekwa kwenye sera hiyo utasaidia watu kusoma wakiwa wanatekeleza majukumu yao mengine kwa kutumia teknolojia ya mtandao.
“Sera hii inaonyesha jinsi tunavyokimbizana na teknolojia kwa kuhamasisha ufundishaji wa mtandao badala ya maandishi ya ubaoni. Hii itasaidia waajiri kubaki na nguvu kazi zao huku wafanyakazi wakiendelea kusoma,” alisema Ally.
Sera mpya ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 pamoja na mitaala iliyoboreshwa inatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Januari 31, 2025, jijini Dodoma.