MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Chama Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wassira, akizungumza na viongozi pamoja na wanaCCM waliojitokeza kumpokea katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM leo Januari 23, 2025 Jijini Dodoma.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Chama Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wassira, akinyanyua Mkuki juu mara baada ya kusimikwa kuma chifu wa kabila la wagogo na kupewa jina la MARUGU(Mpambanaji).
………………….
Atoa maagizo kwa wizara kuchukua hatua
Asisitiza CCM ni kimbilio la wanyonge
Makamu Mwenyekiti wa Chama Chama Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wassira, ameiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhakikisha ardhi ya vijiji iliyoporwa kinyume cha sheria inarudishwa kwa wananchi.
Wassira alitoa maagizo hayo leo, Januari 23, 2025, jijini Dodoma, wakati akizungumza na viongozi pamoja na wanaCCM waliojitokeza kumpokea katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM.
Alisisitiza kuwa Sheria ya Ardhi ya Vijiji inakataza ardhi kuwa bidhaa ya kununuliwa kiholela.
“Wapo watu wajanja… sheria ile inasema ukitaka ardhi ya kijiji zaidi ya ekari 25 lazima wanakijiji wakutane waandike muhtasari na waseme tumekubali. Hata hivyo, lazima faili lifike kwa Rais kisha asaini,” alisema Wassira.
Aliitaka Wizara ya Ardhi kufanya ukaguzi wa ardhi ya vijiji iliyoporwa na kuhakikisha inarudishwa kwa wanakijiji. Alionya kuwa rushwa imekuwa kikwazo, ikiwemo kuhalalisha miliki kwa kutumia majina ya watu waliokufa.
Wassira pia alibainisha kuwa ukiuza ardhi kiholela, masikini hukosa hata pa kukanyaga.
“CCM ni kimbilio la wanyonge. Tutaendelea kuboresha huduma za jamii ili maisha ya wananchi yawe bora zaidi,” alisema.
Aliipongeza serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio makubwa katika sekta za elimu, afya, barabara, na maji.
Katibu wa NEC, Siasa na Oganaizesheni, Issa Gavu, alisisitiza wanachama waendelee kukilinda Chama kwa nguvu zote. Alimpongeza Wassira kwa kuchaguliwa kwa zaidi ya asilimia 98 na wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM.
“Nimuhakikishie kuwa tutaendelea kuhamasisha wanaCCM kufuata maadili ya Chama na kukupa ushirikiano wa kutosha,” alisema Gavu.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adamu Kimbisa, alieleza kuwa hali ya kisiasa mkoani humo ipo shwari, huku wananchi wakionyesha imani kubwa kwa CCM kuelekea uchaguzi mkuu.
“Tumejipanga kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kutokana na utekelezaji mzuri wa ilani ya CCM,” alisema Kimbisa.