DAR ES SALAAM
NA JOHN BUKUKU
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeelezea na kuihamasisha jamii ili kuelewa kuhusu umuhimu wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika (Africa Energy Summit) unaolenga kujadili masuala ya hali ya hewa na jitihada za kupambana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, kupunguza athari zake, na kuharakisha hatua za kukabiliana na mabadiliko hayo.
Mkutano huo unatarajiwa kufanyika tarehe 27-28 Januari 2025, katika Ukumbi wa JNICC, Dar es Salaam, ukiwashirikisha viongozi wa nchi za Afrika pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Akizungumza leo Januari 22, 2025, jijini Dar es Salaam na Full Shangwe Blog kuhusu umuhimu wa mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (PCC), Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema kuwa mkutano huo ni hatua muhimu kwa Afrika, hasa katika kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi na kuongeza kasi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
“Mkutano huu ni mfano mzuri wa jitihada za pamoja. Utachangia kwa kiwango kikubwa katika kupunguza gesi chafuzi na kuongeza ufanisi wa kiuchumi na kijamii barani Afrika,” alisema Dkt. Chang’a.
Aidha, alisifu juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha miundombinu ya hali ya hewa, kuandaa sera madhubuti za kukabiliana na changamoto za tabianchi, na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ndani na nje ya nchi.
“Tunatamani kuona kila mwananchi anapata uelewa wa kina kuhusu umuhimu wa nishati safi na jitihada zinazofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha Bara la Afrika kuimarisha matumizi ya nishati safi ili kupunguza changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Dkt. Chang’a, TMA imejipanga kikamilifu kutoa taarifa za hali ya hewa kwa wakati ili kuhakikisha wageni watakaoshiriki mkutano huo wanapata taarifa zenye uhakika. Alishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya utabiri wa hali ya hewa, hatua inayorahisisha utoaji wa taarifa bora na kwa wakati.