Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amekagua vivuko viwili kati ya sita (6) vilivyowasili katika eneo la Magogoni kwa ajili ya kutoa huduma ya usafiri eneo la Kigamboni na Magogoni na kuagiza kukamilisha taratibu zote za uendeshaji wa vivuko kwa mujibu wa sheria na kanuni za uendeshaji vyombo vya majini nchini.
Ulega amefanya ukaguzi huo leo tarehe 21 Januari 2025, Jijini Dar es Salaam kabla ya vivuko hivyo kuanza kutumika ambapo pamoja na mambo mengine ameshukuru kampuni ya Azam Marine kwa kuingia ubia na Serikali kupitia vivuko hivyo kwani kutapunguza adha ya usafiri katika eneo hilo.
“Nimepata fursa ya kuja kufanya ukaguzi wa vivuko viwili kati ya sita ambavyo tunavitarajia vije kufanya kazi kati ya Magogoni-Kigamboni, na tunashukuru kwa uwekezaji mkubwa unaofanywa na Kampuni ya kizalendo ya Azam Marine”, amesema Ulega.
Ulega ameongeza kuwa ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa Wizara na Taasisi kushirikiana na Kampuni binafsi katika kutoa huduma za kijamii hivyo kuanza kutumia vivuko vipya vya Azam marine kwenye usafirishaji wa abiria katika eneo la Kivukoni ni hatua mojawapo katika uboreshaji wa huduma nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila ameipongeza Wizara ya Ujenzi na TEMESA kwa kuweza kuongeza vivuko viwili (2), ambavyo vitakuwa vinatoa huduma kwa wananachi wa Magogoni – Kigamboni.
Chalamila ameiomba Wizara ya Ujenzi kushirikiana na Shirika la Uwakala wa Meli (TASAC) na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), ili kuweza kuongeza ufanisi wa kazi wa vivuko vipya vinavyokuja viweze kutumika kwa saa 24.
Akizungumza katika ziara hiyo Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala ameeleza kuwa kwa wastani TEMESA inasafirisha ya abiria elfu sitini na tano hadi elfu sabini kwa siku katika eneo la Magogoni na Kigamboni kukiwa na uwepo wa vivuko vitatu lakini hivi karibu idadi ya abiria imepungua kutokana na uwepo wa vivuko viwili tu vinavyotoa huduma.
Kilahala ameongeza kuwa anaamini vivuko hivyo vitakapokuja vitaongeza kasi ya utoaji huduma kwa uharaka na hivyo kuwarahishia wakazi hao usafiri wa haraka.