Wavuvi wadogo wadogo nchini Zanzibar wameshauriwa kuunda vikundi rasmi ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo na kuendeleza shughuli zao za uvuvi kwa tija.
Wito huo umetolewa na Ofisa Uvuvi wa Wilaya Ndogo ya Tumbatu, Amour Sheha Khamis, wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Wavuvi Wadogo Wadogo Zanzibar (ZASFICU), uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo cha Walimu, Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amour alisema uzoefu unaonesha kwamba wajasiriamali wadogo wengi huomba mikopo kwa mtu binafsi, hali inayosababisha changamoto katika upatikanaji wa mikopo hiyo. Alifafanua kuwa kuwa na vikundi rasmi vitakavyotambulika na serikali kutarahisisha utoaji wa mikopo, hasa wanapokuwa waaminifu katika kurejesha mikopo hiyo.
Mwenyekiti wa Muungano wa Vyama vya Ushirika Zanzibar (CUZA), Suleiman Ame Mbarouk, akifungua mkutano huo, aliwahimiza wavuvi kushirikiana ili kufikia fursa nyingi zilizopo baharini kwa maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla.
“Bahari ni chanzo kikubwa cha ajira hasa kwa vijana. Endapo mtashirikiana, mtaisaidia serikali kutekeleza azma yake ya kuboresha maisha ya wavuvi, kama ilivyoelekezwa katika sera ya uchumi wa buluu,” alisema Mbarouk.
Mwenyekiti wa ZASFICU, Omar Moh’d Ali, alieleza kuwa chama hicho kimeendelea kupaza sauti za wavuvi wadogo nchini, kuhakikisha wanapata haki na fursa zinazostahili kupitia shughuli zao za uvuvi.
“Lengo letu ni kuunganisha nguvu na kuwa na sauti moja katika kuhakikisha sera na sheria zinazohusu wavuvi zinaboresha maisha yetu,” alisema Omar.
Kwa mujibu wa Omar, ZASFICU ni muunganiko wa vikundi 57 vya wavuvi, na vikundi vingine vinaendelea na taratibu za kujiunga. Hata hivyo, alibainisha kuwa changamoto ya ukosefu wa ofisi inakwamisha ufanisi wa shughuli zao, hasa kwa upande wa Pemba ambako hakuna ofisi kabisa.
Akizungumzia mapato ya chama hicho, Fatma Abdalla Jaha alieleza kuwa vyanzo vya mapato ni ada za wanachama, fedha za usajili, hisa, na michango. Kwa mwaka 2023-2024, chama kilikusanya shilingi milioni 9,179,000 na kutumia shilingi milioni 4,891,000.
Baadhi ya wavuvi waliohudhuria mkutano huo waliiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Uchumi wa Buluu kuwapatia mafunzo ya kuwasaidia kuhamia uvuvi wa bahari kuu badala ya kubaki katika uvuvi wa kiwango cha chini.
Walitoa wito kwa ZASFICU kuendelea kupigania masuala yao, ikiwemo changamoto za mikopo, sheria, na sera zinazoweza kuboresha maisha ya wavuvi wadogo.
Mkutano huo wa siku moja uliwashirikisha viongozi wa ZASFICU, wataalamu wa masuala ya bahari, maofisa uvuvi, na wanachama wa vikundi mbalimbali vya wavuvi.