Happy Lazaro,Arusha .
Chama cha majaji na mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA) kimefanya mbio za kusherehekea jubilei ya miaka 25 ya chama hicho mkoani Arusha huku wadau mbalimbali wakikumbushwa wajibu wao katika kuunganisha nguvu kwa pamoja na kushirikisha makundi yote ya jamii kwenye kupaza sauti ya kupinga ukatili wa kijinsia.
Aidha tukio hili adhimu lililoandaliwa na
Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) mbali na mbio hizo ni sehemu pia ya harakati zinazolenga kuleta mabadiliko, kuzindua uelewa, na kupinga
masuala ya ukatili wa kijinsia (GBV) yaliyoshamiri na kukithiri katika jamii yetu.
Akizungumza katika mbio hizo kwa niaba ya Spika wa bunge la Tanzania, Dkt.Tulia Ackson ,Mbunge na Mwenyekiti
wa Wabunge wanawake Bunge la Tanzania na pia Mwenyekiti wa Bunge la Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika
(SADC),Shally Joseph Raymond amesema kuwa,Mila gandamizi kama ndoa za utotoni, ukeketaji wa wanawake (FGM), umiliki wa ardhi, nafasi za uongozi na maamuzi bado ni vikwazo katika kufikia usawa wa kijinsia.
Mila na tamaduni potofu ni changamoto kubwa inayopelekea kufisha ndoto za wengi katika kujiletea maendeleo ya kweli.
Ameongeza kuwa juhudi za
pamoja na mbinu mbalimbali za kujikwamua kutoka katika
madhila haya zinafanyika ili kubomoa mifumo gandamizi na kuvunja minyororo iliyojikita katika jamii zetu kwa karne nyingi.
“Hivyo jubilei ya TAWJA ni tukio linalostahili kusherehekewa, siyo tu kwa sababu ya umri bali dira na dhima ya Chama tangu awali,kuwa mshumaa wa mwanga na matumaini, ikipigania haki za
kijinsia, hususani za wanawake na Watoto”amesema.
“Tunaposherehekea tukio hili kubwa, huku tukijivunia mafanikio yetu, inatupasa kutafakari kwa pamoja changamoto
zinazotukabili kama jamii.”amesema .
Amefafanua zaidi kuwa, wakati jitihada
hizi zikiendelea bado jamii zetu zimezungukwa na mila, tamaduni
na mifumo gandamizi na nyingi zikiwa zimepitwa na wakati.
“Wanawake na watoto bado wapo nyuma katika kulinda na kuteteta haki zao za msingi,hii inatukumbusha kuwa
mapambano haya si tu ni ya kinadharia bali yanasura ya uhalisia inayohitaji tafakuri na mikakati ya kina katika kuyatatua. “ameongeza.
Ameongeza kuwa, ushiriki wa wenzetu wanaume ni nyenzo muhimu katika kubadilisha fikra na mitazamo hasi dhidi ya
wanawake.
Ameongeza kuwa ,pamoja na ukweli kuwa mabadiliko si rahisi kupokewa, sauti na mikakati ni muhimu ili kufikisha ujumbe
sahihi, Wanawake Majaji na Mahakimu wamepata upendeleo wa kipekee kupata elimu na upeo (exposure) na wote wakiwa katika ngazi ya maamuzi na hivyo kuwa kichochezi kikubwa cha kuleta mabadiliko hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuwavuta na kuwatetea.
“Mbio hizi za TAWJA zenye kaulimbiu “Mshikamano katika Haki za Kijinsia Huanzia Hapa: Shiriki na Elimisha.”
zinatukumbusha umuhimu wa kuunganisha nguvu zetu na kushirikisha makundi yote ya jamii kwenye kupaza sauti ya kupinga ukatili wa kijinsia.”amesema .
Ameongeza kuwa ,kupitia mbio hizi, imenidhihirishia jinsi Chama kilivyoweza kufikisha ujumbe kwa jamii juu ya athari
na madhila ya ukatili wa kijinsia na kimeweza pia kuunganisha sauti za kukemea na kwa kukimbia kwa pamoja kama kaulimbiu za mbio hizi zinavyosema
Tunaposhiriki mbio hizi za Jubilei ya Miaka ishirini na tano (25) ya TAWJA.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha majaji na mahakimu wanawake wa Tanzania (TAWJA) ,Berke Sehel amesema kuwa, Mbio hizi ni ishara ya kuanza maadhimisho ya Jubilei ya
miaka 25 ya TAWJA yenye kaulimbiu “Kusherehekea Utofauti na Mshikamano katika Usawa wa Kijinsia.”ambapo dhumuni hasa ya mbio hizi sio tu ni kwa ajili ya kuchangamsha viungo vyetu, bali
pia kuwashirikisha, kuhamasisha na kuunda uelewa kwa jamii na umma kuhusu hatua za kuchukua dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia (GBV) dhidi ya wanawake na watoto na kuonyesha kwa vitendo mshikamano wetu na dhamira yetu ya kudumisha haki na usawa wa kijinsia nchini Tanzania,Mjumuiko huu wa leo ni uthibitisho tosha wa nguvu ya pamoja ya kutetea na kukuza haki za wanawake na watoto nchini.
Sehel amesema kuwa, baada ya kukimbia leo, wanachama wa TAWJA watapata
wasaa wa kutembela shule za Shule za Sekondari sita, ambazo ni
Ilboru, Arusha, Kimandolu, Kaloleni, Muriet na Sinoni kwa ajili ya kuanzisha Klabu za Haki za Kijinsia Mashuleni ambapo Wanachama wa TAWJA watapata fursa ya kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu kutambua aina zote za ukatili wa
kijinsia, jinsi na wapi ya kuripoti ukatili wa kijinsia na kuwapa ujuzi muhimu wa maisha ikiwemo kuweka malengo ya kibinafsi na kujali afya na usafi wao.
“TAWJA imekuwa ikijikita kwenye kukuza haki za binadamu na usawa kwa wote, hususan kwa wanawake, watoto na
makundi maalum. Kwenye kuadhimisha Jubelei ya miaka 25, TAWJA inajivunia kwa hatua kubwa ilikofokia kwani imeweza
kuletea mchango chanya kwenye jamii kwa upande wa haki, kwani TAWJA imechangia kwenye mabadiliko ya Sheria ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa pamoja na kuchukua juhudi za
makusudi za kutoa elimu kwa wadau wa haki jinai, wabunge na jamii, kuhusu rushwa ya ngono (sextortion) na hivyo kuleta uelewa mpana katika jamii juu ya uwepo na athari ya vitendo vya rushwa ya ngono na hatimaye kubadilishwa kwa sheria kwa kuongeza kifungu maalum kuhusiana na rushwa ya wanawake”amesema.