Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete akizungumza katika mkutano mkuu maalum wa CCM unaofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na viongozi mbalimbali katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Taifa uliofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma tarehe 19 Januari, 2025.
……………..
Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete ameonyesha hekima ya hali ya juu na uzoefu wake katika siasa kwa kutoa ushauri thabiti unaolenga kuimarisha umoja na uwazi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza leo katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM mjini Dodoma, ulioongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Kikwete amesisitiza umuhimu wa kufuata utaratibu rasmi wa chama kwa kupitisha azimio la kuidhinisha majina ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, kama wagombea wa urais wa mwaka 2025.
Katika hotuba yake, Kikwete amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na viongozi hao na kueleza kuwa ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao hauna shaka kutokana na mafanikio yaliyopatikana.
“Kama tumekubaliana katika mkutano huu, basi Rais Samia na Rais Mwinyi wanaelekea kushinda tena kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Lakini ni muhimu tupitishe azimio rasmi ili kuhakikisha tunazingatia taratibu za chama na kutoa ujumbe wa mshikamano kwa wanachama wote,” alisema Kikwete.
Kwa kuhitimisha, Kikwete aliwatia hamasa wajumbe kwa kuanzisha wimbo wa kuonyesha imani kwa Rais Dk. Samia na Dk. Mwinyi, ambao ulizua shangwe kubwa katika ukumbi wa mkutano.
Hatua hii ya Rais Mstaafu Kikwete imeonyesha uzalendo na umakini wake katika kulinda mshikamano wa CCM, huku ikisisitiza umuhimu wa kuheshimu misingi ya kidemokrasia na taratibu ndani ya chama