DAR ES SALAAM
NA JOHN BUKUKU
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wamejipanga kuhakikisha miundombinu ya barabara inapitika, ikiwemo barabara ya mwendokasi kutoka Gongo la Mboto hadi Kamata, kabla ya Marais wa nchi mbalimbali kuwasili nchini kushiriki Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika utakaofanyika Januari 27-28, 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Meneja wa TANROADS Mradi wa BRT, Mhandisi Frank Mbilinyi, amesema wamejipanga kukamilisha ujenzi wa barabara ya BRT awamu ya tatu kwa wakati ili kuhakikisha wageni wanapokelewa kwenye mazingira mazuri.
“Barabara ya Nyerere ni lango kuu la kuingilia nchini, na wageni wengi kutoka nje ya nchi wanaitumia barabara hiyo. Tumesisitiza usafi na kuhakikisha maeneo yote yanapitika,” amesema Mhandisi Mbilinyi.
Ameeleza kuwa barabara hiyo imekamilika kwa sehemu kubwa, na maeneo madogo yaliyobaki yanafanyiwa kazi. Pia, wameanza kuweka taa za barabarani kutoka uwanja wa ndege hadi mjini ili kuboresha mwonekano wa miundombinu kabla ya mkutano kuanza.
Aidha, Mhandisi Mbilinyi amesema hatua za makusudi zimechukuliwa kuhakikisha usafi wa barabara unafanyika kwa kufagia vumbi, kuondoa vifusi na mchanga.
Amewataka Watanzania kuwa tayari kupokea ugeni huo mkubwa, akisisitiza kuwa ni fursa ya kiuchumi kwa taifa. “Wito wangu kwa Watanzania ni kutunza miundombinu ya barabara, kwani inajengwa kwa manufaa ya wananchi wenyewe,” amesisitiza.