Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Visiwa vya Comoro Mheshimiwa Saidi Yakubu amekutana na kufanya mazumgumzo na Rais wa Umoja wa Visiwa vya Comoro Mheshimiwa Azali Assoumani tarehe 16 Januari, 2025, Ikulumjini Moroni.
Mazungumzo hayo yalilenga kubainisha mikakati na mipango ya ushirikiano kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro kwa mwaka 2025.
Akizungumza katika kikao hicho , Mheshimiwa Balozi Saidi Yakubu alimshukuru Mheshimiwa Rais Azali Assoumani na Serikali yake kwa ushirikiano iliompatia mwaka 2024 ambapo alieleza kuwa ushirikiano huo umeuwezesha Ubalozi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi wa hali ya juu.
Alibainisha kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Mei hadi Desemba 2024, Ubalozi ulifanikisha matukio mbalimbali yenye tija kwa wananchi kutoka nchi mbili hizi na kutolea mfano kufanyika kwa Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiao uliofanyika Mwezi Julai 2024 jijini Dar es Salaam na mikataba mbalimbali ilisaniwa.
Mheshimiwa Balozi Yakubu aliongeza kuwa Ubalozi uliratibu Kongamano la Biashara na Uwekezaji katika sekta za kilimo, mifugo na usafirishaji ambapo wafanyabiashara na wajasiriamali wa nchi hizo walipata nafasi ya kubuni mikakati ya kushirikiana.
Mheshimiwa Balozi Saidi Yakubu alisema Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro kwa mwaka 2025 umelenga kuendelea kuimarisha ushirikiano kupitia nyanja za kiuchumi na kijamii, kuvutia wawekezaji pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binfasi za nchi hizo.
Vile vile, alibainisha kuwa Tanzania ipo tayari kuipatia Comoro vitabu na nyenzo za kufundisha somo la Kiswahili iwapo somo hilo litatambuliwa katika mtaala yao.
Naye Mheshimiwa Rais Azali Assoumani kwa upande wake alipongeza juhudi zinazochukuliwa na Ubalozi katika kuimarisha ushirikiano katika nyanja za kiuchumi na kijamii na kuongeza kuwa juhudi zinazochukuliwa zinathibitisha undugu uliopo kati ya wananchi kutoka Mataifa haya.
Alihimiza Ubalozi kuendelea kuvutia wawekezaji kutoka Tanzania kuhamishia shughuli zao nchini Comoro ili kusaidia maendeleo.
Akigusia suala la lugha ya Kiswahili, Mheshimiwa Rais Azali alisema Tanzania ni rafiki wa kweli kwa Comoro hivyo Serikali yake itaendelea kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo kufundisha somo la Kiswahili.
Aliongeza kuwa lugha ya Kiswahili itasaidia kuunganisha wafanyabiashara na wananchi wa Comoro wanaotembelea Tanzania.
Mazungumzo baina ya Mheshimiwa Rais Azali Assoumani na Mheshimiwa Balozi Saidi Yakubu yamethibitisha azma na nia ya dhati iliyonayo Serikali ya Comoro katika kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na Tanzania. Hali hii inabainisha fursa zilizopo kwa raia wa Mataifa haya mawili kuendeleza miradi ya uzalishaji na kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali.