DAR ES SALAAM
Taasisi ya Makumbusho ya Taifa la Tanzania (NMT) imeweka mkazo katika kuimarisha utalii wa kihistoria na utamaduni wa Tanzania kupitia fursa ya ugeni wa Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika, unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 na 28 Januari jijini Dar es Salaam.
Katika mahojiano maalum na kituo cha Star TV mapema leo, Mhifadhi Historia Bw. Shomari Rajabu na Afisa Utalii Bi. Antonia Mnkama walielezea maandalizi ya NMT katika kunufaika na tukio hili kubwa. Walibainisha kuwa mkutano huu ni jukwaa muhimu kwa Tanzania kuonyesha vivutio vya kihistoria na utamaduni kwa wageni wa kimataifa.
“Tunatarajia kutumia nafasi hii kutangaza historia tajiri ya Tanzania, ikiwemo vivutio vyetu vilivyopo jijini Dar es Salaam kama Kijiji cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni,” alisema Bw. Shomari Rajabu.
Kwa mujibu wa maelezo yao, Makumbusho ya Taifa imeandaa programu maalum za kuwatembeza wageni wa mkutano huu katika maeneo ya kihistoria, zikiwemo maonyesho ya utamaduni wa makabila mbalimbali na historia ya Tanzania, lengo likiwa ni kuwajengea wageni ufahamu wa kina kuhusu urithi wa taifa.
Akiongeza hoja, Bi. Antonia Mnkama alisema, “Hii ni fursa adimu kwa wageni wa Afrika kutembelea na kujifunza urithi wetu wa historia, huku tukionyesha namna utamaduni wetu unavyoweza kuchangia maendeleo ya utalii wa kiutamaduni na kihistoria.”
Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika unatarajiwa kuwaleta viongozi, wawekezaji, na wadau wa sekta ya nishati, huku Tanzania ikijikita pia kutumia tukio hili kuimarisha mahusiano ya kikanda kupitia historia na utalii wake.