Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) limehimizwa kuchukua hatua madhubuti katika kuhakikisha Kamusi ya Kiswahili inatumika ipasavyo shuleni ili kuimarisha matumizi sanifu ya lugha ya Kiswahili kwa watoto wa Kitanzania.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi, alitoa rai hiyo leo, Januari 14, 2025, alipokuwa akitembelea ofisi za BAKITA jijini Dar es Salaam. Waziri Kabudi alisisitiza kuwa kamusi ni nyenzo muhimu katika kujenga msingi bora wa Kiswahili fasaha miongoni mwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
“Kamusi siyo tu kitabu cha kiada bali ni msingi wa kuhifadhi na kukuza lugha yetu. Ni jukumu letu kuhakikisha kila mwanafunzi wa Kitanzania anafahamu matumizi ya kamusi tangu ngazi ya shule ya msingi,” alisema Waziri Kabudi.
Aliongeza kuwa matumizi ya kamusi yatawasaidia watoto kujifunza Kiswahili sahihi, hatua inayowaandaa kwa ajira mbalimbali kama vile uandishi wa habari, ualimu, na sekta nyingine zinazohitaji mawasiliano bora.
Prof. Kabudi alilitaka BAKITA kuanzisha mkakati wa kitaifa wa kuhamasisha matumizi ya kamusi shuleni, akisema:
“Tukianzisha utamaduni huu mapema, tutakuwa tumetengeneza kizazi kinachoheshimu lugha yake na kutumia Kiswahili fasaha katika kila sekta.”
Aidha, alihimiza BAKITA kuanzisha programu maalum kwa wageni wanaoingia nchini ili kuwajengea uwezo wa kutumia Kiswahili sanifu, hasa wale wanaokuja kwa shughuli za uwekezaji na elimu.
Katika sekta ya sanaa, Waziri Kabudi aliwahimiza wasanii wa filamu na muziki kushirikiana na BAKITA kwa ajili ya mapitio ya kazi zao ili kuhakikisha Kiswahili sanifu kinatumika.
“Sanaa ni kioo cha jamii, hivyo ni lazima kazi zote za wasanii zizingatie matumizi sahihi ya lugha,” alieleza.
Ziara hiyo ililenga kutathmini utendaji wa BAKITA na kujadili njia za kuendeleza Kiswahili kama lugha ya kitaifa na kimataifa.