Wafanyabiashara wakiwa ukumbini kwenye kikao
……….
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Baadhi ya wafanyabishara Mkoani Mwanza wametoa maoni juu ya ukusanyaji bora wa kodi nchini ili waweze kufanya shuguli zao vizuri.
Maoni hayo wameyatoa leo Jumatatu tarehe 13 januari, 2025 kwenye Kikao cha wadau cha Kukusanya, kupendekeza na kuwasilisha changamoto za masuala ya kodi nchini kilicholenga kuboresha namna bora ya pamoja ya kufikia malengo.
Sijaona James ni msemaji wa Chama cha wavuvi Tanzania amesema watu wanaohusika na ukusanyaji wa kodi wanachukua rushwa badala ya Kodi hatua inayopelekea serikali kukosa mapato.
Pia ameiomba Serikali kutengeneza Wizara ya ujasiliamali na ukuzaji mitaji kwaajili ya kuwafatilia wajasiriamali na kuwashauri namna ya kukuza mitaji yao.
Kwaupande wake Dkt.Felician Ndauzi kutoka kituo cha afya Huduma kilichopo Kilimahewa Mkoani hapa, amesema utitiri wa kodi umekuwa kikwazo kwa wafanyabishara hivyo Serikari inapaswa kuingilia suala hili ili wafanyabishara waweze kumudu gharama za kulipia kodi.
Naye Nyiriza Makongoro, amesema mwenendo wa ukusanyaji wa kodi nchini siyo rafiki kwenye sekta ya bishara kutokana na muda mwingine wanalipia kodi ambazo siyo sahihi.
Mwenyekiti wa Chemba ya wafanya biashara Mwanza (TCCIA) Gabriel Chacha ametoa wito kwa serikali kuondoa mfumo wa kukokotoa kodi ambao sio rafiki kwani haufuti taarifa za nyuma za uhai wa biashara na waondoe utitiri wa kodi kwenye biashara badala yake zilipwe kwenye mwamvuli mmoja.
“Changamoto nyingine ni sheria, faini na tozo hapa wafanyabiashara wanaumizwa sana na zinapaswa kupitiwa upya na kuzirekebisha maana adhabu zimewekwa kwa kiwango kimoja ambacho kinawaumiza moja kwa moja wajasiriamali.” Ameongeza Bwana Chacha
Awali akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kukusanya maoni ya maboresho ya Kodi Mhe. Balozi Ombeni Sefue ametoa rai kwa wafanyabiashara Mwanza kujenga tabia ya kulipa kodi ili kuipa nguvu serikali na kuhakikisha inaweza kujitegemea kwa kuboresha miundombinu mathalani ya Afya.
“Tanzania tija yetu ya kukusanya mapato bado ni ndogo ni kati ya asilimia 12 hadi 13 tu na haipaswi kuwa kuwa hivyo maana angalau tufikie asilimia 16 maana wananchi wanataka shule zijengwe, miundombinu ya afya iwepo tena ya kisasa je tutafikaje huko kama hatutakua na fedha.” Mwenyekiti.
Tume hiyo imeundwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kupokea maoni ya wadau juu ya kuwa na mfumo bora wa kukusanya mapato nchini pasipo malalamiko.