Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Komredi Kheri James, amepongeza juhudi za uongozi, watumishi, na wananchi wa Manispaa ya Iringa kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.3 inayotekelezwa katika Manispaa hiyo.
Pongezi hizo zilitolewa leo wakati wa ziara ya kikazi ya Mkuu huyo wa Wilaya alipotembelea Kata sita za Kitwiru, Ruaha, Isakalilo, Kwakilosa, Mwangata, na Nduli kwa lengo la kukagua maendeleo ya miradi hiyo na kuhamasisha uwajibikaji.
Akizungumza katika maeneo aliyotembelea, Komredi Kheri James alisema:
“Nimefurahishwa na ubora wa ujenzi wa miradi hii unaozingatia viwango na kuheshimu muda uliopangwa. Hili ni jambo la kujivunia kwani linaonyesha dhamira ya dhati ya kuharakisha huduma kwa wananchi wa Iringa.”
Komredi James aliwaelekeza wasimamizi wa miradi kuhakikisha kila mradi unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaostahili ili huduma zilizokusudiwa ziwafikie wananchi bila kuchelewa. Pia aliwataka wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuhakikisha wanakamilisha kazi kwa mujibu wa mikataba yao.
Mbali na ukaguzi wa miradi, Mkuu wa Wilaya alitembelea shule mbalimbali za msingi na sekondari katika Manispaa ya Iringa kufuatilia zoezi la upokeaji wa wanafunzi. Alionyesha kuridhishwa na utaratibu mzuri wa mapokezi na usajili wa wanafunzi, akisisitiza umuhimu wa elimu kama nguzo ya maendeleo ya jamii.
Ziara hiyo imeonyesha dhamira ya kuimarisha maendeleo na uwajibikaji wa pamoja kati ya viongozi, wakandarasi, na wananchi katika kujenga Iringa imara.