Katika kipindi cha Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Serikali, Wasemaji wa Vyombo vya Usalama, Taasisi na Maafisa Habari wametakiwa kutumia nguvu yao ya Mawasiliano kuwafanya Watanzania washiriki na kuvuka kwenye Uchaguzi Mkuu kwa furaha kwa kutumia maarifa yao katika kuwaelimisha wananchi kuzingatia na kutii sheria bila shuruti wakati wakitekeleza haki yao Kikatiba ya kuchagua au kuchaguliwa kwa amani na utulivu.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akifunga Kikao Kazi cha Mwaka cha Wasemaji wa Vyombo vya Usalama na Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, tarehe 11 Januari 2025 jijini Dodoma
“Tutumie nguvu sasa kuelimisha ili wakati wa uchaguzi Wananchi waweze kushiriki katika zoezi hili kwa utulivu mkubwa wakiwa na furaha”Katibu Mkuu Msigwa amesema
Msigwa amesisitiza suala la wadau mbalimbali wa uchaguzi wanaogombea na wasiogombea waelekezwe haki zao na mambo ambayo hawapaswi kuyafanya kwani wakiyafanya watakuwa wamekanyaga usalama wa raia na mali zao.
Kikao hicho kilienda sambamba na kuzindua Mikakati ya Mawasiliano ya Wizara na Vyombo vyake vya Usalama tarehe 9/1/2025 ambapo Msigwa ameahidi kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa mikakati hiyo kwani hayo ni maelekezo ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Nitafuatilia kwelikweli na mimi sipo tayari kuona maelekezo ya Rais hayatekelezwi” Alisema Msigwa
Pia, amebainisha mpango wa kukutana na Wakuu wa Vyombo vya Usalama kwa lengo la kujadiliana nao kutengeneza mazingira rafiki ya Vitengo vya Habari na Mawasiliano ili mawasiliano yawe yenye tija, na kazi iwe ni kutumia maarifa badala ya nguvu.
Kwa Upande wake, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bi. Christina Mwangosi amesema lengo la kikao hicho ni kufanya tathmini ya utendaji kazi wa Vitengo vya Habari ambapo kikao cha kwanza kilifanyika mwaka wa fedha 2023/2024 kiliwekwa maazimio 10 kati yake Nane yametekelezwa, miongoni mwa maazimio yake yalikuwa ni uandaaji wa mikakati ya Mawasiliano ya Wizara na Vyombo vyake.
“Kuzinduliwa kwa mikakati hii ya Mawasilino kwetu sisi ni chachu na fursa ya kuboresha utendaji kazi wetu, kwani itatusaidia kutelekeza shughuli za mawasiliano na habari kwa umma ambayo tumejipanga wenyewe”. Alisema Bi Christina.
Kikao kazi hicho kimechukua siku tatu ambacho kilitanguliwa na Uzinduzi wa Mikikati ya Mawasilino ya Wizara na Vyombo vyake Usalama tarehe 9, Januari ilienda sambamba na mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wa Maafisa habari katika kutekeleza majukumu yao kuhabarisha Umma.