Wasafirishaji wa abiria kwa kutumia Pikipiki maarufu kama Bodaboda wametakiwa kutojichukulia sheria mkononi pindi linapotokea tukio la uhalifu kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na badala yake watoe taarifa kwa Jeshi la polisi ili hatua za kisheria ziweze chukuliwa dhidi ya wahalifu hao.
Kauli hiyo ilitolewa Januari 10, 2025 na Polisi Kata ya Halungu Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Miccah Mtafya wakati alipokuwa anatoa elimu juu ya madhara ya kujichukukia sheria mkononi katika Kijiwe cha Mitendo kilichopo Kijiji cha Halungu Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe.
Naye, Mwenyekiti wa Kijiwe hicho Yusuph Joba Joba amewaomba bodaboda hao kushiriki kamilifu katika shughuli za ulinzi shirikishi katika Kata hiyo ili kupunguza wimbi la uhalifu.
Sambamba na hilo, Mkaguzi Mtafya ametaka jamii kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu pindi unapojitokeza kwa wakati, ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa haraka.